Muhammad Mokhber amesema hayo katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin wa Russia pambizoni mwa Kikao cha Viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan, ambapo wamesisitiza udharura wa kupanuliwa uhusiano kati ya Tehran na Moscow.
Mokhber ameeleza bayana kuwa, mwenendo wa uhusiano wa nchi mbili hizi uko katika mwelekeo sahihi na unakwenda kwa kasi inayofaa. Amesema Iran na Russia zinajivunia uhusiano wa kina, wa kimkakati, usiobadilika na ambao unaathiri matukio yanayoendelea kushuhudiwa duniani.
Huku akiashiria kuridhishwa kwake na maendeleo ya utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na Moscow, Mokhber amesema uhusiano wa kistratijia wa pande mbili hautabadilika.
Kaimu Rais wa Iran ameongeza kuwa, ukurasa mpya umefunguliwa katika uhusiano kati ya Tehran na Moscow ambao utakuwa na manufaa si tu kwa pande hizo mbili bali pia kwa eneo na dunia nzima.Putin kwa upande wake ameeleza kuridhishwa kwake na mchakato wa ushirikiano wa pande mbili, na kusema Moscow inazingatia suala la kupeleka mbele ajenda hiyo kwa kushirikiana na Iran.
Aidha Rais wa Russia amesema nchi yake ina uhusiano wa kirafiki, uliokita mizizi na usiobadilika na Iran, huku akisisitizia haja ya kuendeleza ushirikiano wa pande mbili hususan katika sekta za uchumi na biashara.