Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo leo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, jinai za kivita na kuwaua kwa umati Wapalestina hasa watoto wadogo wasio na hatia, ni jinai kubwa mno zinazofanywa na Wazayuni ambazo mwanadamu yeyote hawezi kuziunga mkono.
Amesema, wale waungaji mkono wakaidi zaidi wa utawala wa Kizayuni wanaendelea kula matapishi yao wakati wanapodai kuwa ni viranja wa kupigania haki za binadamu katika nchi nyingine, kumbe wao ndio wauangaji mkono wakuu wa jinai za kutisha wanazofanyiwa Wapalestina kila siku na wanajeshi makatili wa Israel.
Jinai hizo hazifanyiki Ghaza tu, bali katika maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, kama Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, nako pia utawala wa Kizayuni unafanya jinai kila siku dhidi ya Wapalestina.
Taarifa zilizotolewa juzi zilisema kuwa, Wapalestina watano wa mji wa Jenin ni miongoni mwa makumi ya Wapalestina waliouawa shahidi kwa kupigwa risasi na kushambuliwa kwa mabomu na jeshi la utawala wa Kizayuni.
Juzi Jumamosi, shirika la habari la WAFA lilimnukuu Wissam Bakr, Mkrugenzi wa Hospitali ya Serikali ya Jenin akisema kuwa, Wapalestina hao waliuawa shahidi Ijumaa katika uvamizi wa wanajeshi makatili wa Israel huko Jenin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
342/