Rais Abdul Latif Rashid wa Iraq amezungumza kwa simu na Rais mteule wa Iran, Masoud Pezeshkian, na kumpongeza kwa kuibuka na ushindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais, Ijumaa iliyopita.
Rais wa Iraq amesema kuwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq ni mkubwa, imara na kwa ajili ya maslahi ya nchi mbili na kusisitiza hamu ya nchi yake ya kulinda na kuboresha uhusiano na pia kuandaa mazingira ya kushirikiana zaidi nchi mbili katika serikali mpya ya Iran.
Kwa upande wake, Rais mteule wa Iran ameshukuru kwa salamu za pongezi kutoka kwa wananchi na serikali ya Iraq na kutoa mwito wa kupanuliwa ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kidini kati ya nchi mbili. Dakta Masoud Pezeshkian amesema anataraji kuwa uhusiano huo utaimarishwa na kupanuliwa zaidi katika kipindi kipya kwa ushirikiano wa maafisa wa ngazi za juu wa nchi mbili. Rais mteule wa Iran amepongeza juhudi za Rais wa Iraq za kustawisha uhusiano wa pande mbili na kusema: Nchi mbili za Iran na Iraq zina mitazamo na misimamo ya pamoja katika nyanja nyingi jambo ambalo ni msingi mzuri wa kupanua uhusiano na kustawisha ushirikiano kati ya pande mbili.
342/