Main Title

source : Parstoday
Jumatano

10 Julai 2024

15:16:30
1471080

Jeshi la Israel ndilo jeshi lenye maadili machafu zaidi duniani

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, jeshi la Israel ndilo jeshi lenye maadili machafu zaidi duniani na kusisitiza kuwa, uungaji mkono wa Hizbullah kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Ghaza utaendelea hadi taifa la Palestina litakapojikomboa.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Sayyid Hassan Nasrullah akisema hayo wakati wa mkesha wa mwezi mtukufu wa Muharram na kusisitiza kuwa, miezi kadhaa imepita na hakuna misaada yoyote iliyoruhusiwa kuingia kwenye ukanda wa Ghaza na jambo hilo limesababisha maafa katika ukanda huo.

Vile vile amesema, swali linalojitokeza hapa ni kwamba, je, ni jambo linaloingia akilini kuachiwa hali hiyo ya Ghaza iendelee?

Amesema, kila Muislamu mwenye akili timamu anajiuliza maswali bila ya kupata majibu kwamba nchi za Kiarabu na Kiislamu ziko wapi? Hivi ni kweli haziwezi kufanya chochote cha kuwaokoa wananchi wa Palestina hasa wa Ghaza? 

Katibu Mkuu huyo wa Hizbullah ya Lebanon pia amesema: Sisi tunaamini kwamba ni jukumu letu kutekeleza wajibu wetu. Kila siku watu wetu wanauawa shahidi katika njia ya kuliunga mkono Taifa la Palesina na ukombozi wa Quds, na tunajifakharisha na kujivunia kwa hilo. Tutaendelea na njia hiyo hadi malengo yatakapofikiwa.

Sayyid Hassan Nasrullah pia amesema, kambi inayowasaidia watu wa Ghaza ambayo iko Lebanon, Iraq na Yemen pamoja na waungaji mkono wakuu wa ukombozi wa Palestina kama Syria na Iran wanawaonesha walimwengu wanaopenda haki, taswira inayofurahisha. Lakini vitendo vya baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu kuhusu Ghaza vinatia kinyongo.

Aidha amesema, kila wakati mmoja wetu anapouawa shahidi au tunapotishiwa kushambuliwa kwa vita, hatutishiki, bali tunazidi kuwa imara katika imani na misimamo yetu.

342/