Dkt. Hadi Farajvand, balozi wa Iran nchini Uholanzi amesema hayo katika kikao cha 106 cha Baraza la Utendaji la Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali na kubainisha kwamba, waliohuusika katika kuunga mkono silaha za kemikali wanapaswa kutiwa mbaroni na kupandishwa mahakamani.
Balozi wa Iran nchini Uholanzi amesema hayo sambamba na kumbukumbu ya mashambulizi ya silaha za kemikali katika mji wa Sardasht nchini Iran na kusisitiza kwamba, watenda jinai hao wanapaswa kushtakiwa mara moja katika mahakama za kimataifa.
Balozi Farajvand aidha amesema, vikwazo dhidi ya Iran na kuzuia usambazaji wa dawa na vifaa vya matibabu vinavyohitajika na maveterani wa silaha za kemikali vinakiuka mkataba na sheria za haki za binadamu.Hivi karibuni pia Ali Bagheri Kani Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema katika siku ya kumbukumbu ya mashambulizi ya silaha za kemikali katika mji wa Sardasht nchini Iran kwamba: Wale waliounga mkono jinai za utawala wa Saddam Hussein dhidi ya watu wa Sardasht nchini Iran hivi sasa wanaunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza. Utawala wa Baath wa Iraq Juni 28 mwaka 1987 ulitumia mabomu ya kemikali kushambulia maeneo manne ya kaunti ya Sardasht katika mkoa wa Azerbaijan Magharibi, unaopatikana kaskazini magharibi mwa nchi. Raia 119 wa eneo hilo waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 8,000 walidhurika kwa gesi ya sumu na kupata maradhi ya aina mbalimbali.
342/