Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

11 Julai 2024

15:56:51
1471303

Azma ya Pakistan ya kuimarisha uhusiano wa pande zote na Iran

Muhammad Shahbaz Sharf Waziri Mkuu wa Pakistan amesisitiza katika mazungumzo ya simu na Masoud Pezeshkian Rais Mteule wa Iran kuwa Islamabad iko tayari kustawisha uhusiano na Tehran. Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa mapatano yaliyofikiwa na nchi mbili katika ziara ya mwezi Aprili ya Rais Shahidi Raisi wa Iran huko Pakistan ni nukta muhimu katika uhusiano wa pande mbili.

Shahbaz Sharif amempongeza Pezeshkian kwa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais wa Iran na kuongeza kuwa Islamabad ina hamu ya kushirikiana kwa karibu na serikali mpya ya Tehran ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi mbili na kukuza ushirikiano wa pande zote katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, nishati na usalama wa kikanda. Katika amzungumzo hayo ya simu naye Masoud Pezeshkian Rais mteule wa Iran amemshukuru Waziri Mkuu wa Pakistan kwa salamu za pongezi na akabainisha hamu yake ya kukuza zaidi uhusiano mkongwe uliopo kati ya mataifa haya mawili. Muhammad Ishaq Dar Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan pia juzi Jumanne alitoa matamshi sawa na haya kwamba: 'Kufuatilia na kutekeleza mapatano yaliyosainiwa katika ziara ya Aprili iliyopita ya Rais Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran nchini Pakistan baada ya kuundwa serikali mpya Tehran kutapelekea kuongezeka mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi mbili na kufikia kiwango kinachotarajiwa cha dola bilioni 10 kwa mwaka.'

Matamshi ya Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa  Pakistan kuhusu hamu ya nchi hiyo ya kukuza uhusiano na Iran inadhihirisha ushirikiano mwema na wa uaminifu wa Iran na majirani zake, Waislamu na kanda hii kwa ujumla, suala ambalo limezipelekea aghalabu ya nchi za eneo ziitambue Iran kama nchi rafiki na inayolitakia heri  eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima kwa ujumla. Hii ni katika hali ambayo, sambamba na kuwepo uhusiano wa kisiasa wa kiwango cha juu kati ya Tehran na Islamabad; viongozi wa Pakistan wanauhesabu uwezo na suhula za kiuchumi za Iran katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika sekta ya nishati kuwa fursa mzuri kwa ajili ya kupanua uhusiano na kudhamini mahitaji ya nchi hiyo. Mkabala wake, Iran pia ambayo ililiweka katika vipaumbele vya sera zake za nje khususan katika serikali ya Shahidi Raisi suala la kustawisha uhusiano wa pande zote na nchi jirani na kanda hii; katika miaka ya karibuni imechukua hatua athirifu kwa ajili ya kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati yake na nchi za eneo khususan Pakistan. 

Katika uga wa nishati, Iran imetekeleza majukumu yake katika kalibu ya makubaliano kati yake na Islamabad kwa ajili ya kuuza gesi kwa kuandaa miundomsingi muhimu ya kupeleka gesi Pakistan ikiwa ni pamoja na kukamilisha utandazaji wa mabomba hadi katika mpaka wa nchi hiyo. Wakati huo huo uwezo mbalimbali wa Iran wa kuzalisha bidhaa zenye ubora pia umeipelekea Pakistan ipanue masoko yake ya mpakani kwa kuzingatia kuwepo mpaka mrefu wa pamoja kati ya nchi mbili. Pakistan ina mpaka wa pamoja na Iran kupitia mkoa wa Baluchistan na inafanya kila iwezalo kuweka miundombinu inayohitajika ikiwemo kukuza masoko ya maeneo ya mpakani kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa kibiashara kupitia nchi kavu mipakani. Bila shaka Iran na Pakistan zina uhusiano mkubwa kwa kuzingatia mafungamano ya kidini, kilugha na kiutamaduni yaliyopo kati yao. Kwa ibara nyingine tunaweza kusema kuwa Iran ni mshirika wa kimkakati wa Pakistan. Kwa sababu hiyo Islamabad kivyovyote vile haitaki kuona mivutano ikijiri kati yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na inatabiriwa kuwa nchi mbili katika siku zijazo pia zitachukua hatua kubwa zaidi ili kukuza uhusiano khususan katika upande wa usalama. Iran na Pakistan pia hazitatoa mwanya kwa makundi ya kigaidi na waibua machafuko kuvuruga usalama wa eneo na uthabiti katika uhusiano wa Tehran na Islamabad. 


342/