"Chini ya utawala wangu, tutatanguliza mbele suala la kuimarisha uhusiano na majirani zetu," Pezeshkian ameandika katika makala iliyochapishwa na Tehran Times, jana Ijumaa.
Amengeza kuwa: "Tutatetea kuanzishwa kwa 'kanda yenye nguvu' badala ya eneo ambalo nchi moja inataka kuzidhibiti nchi nyingine."
Pezeshkian, aliyekuwa daktari wa upasuaji wa moyo na waziri wa afya, ameandika kwamba anaamini kwa uthabiti kuwa “mataifa jirani na yenye undugu hayapaswi kupoteza mali zao zenye thamani kwa mashindano ya kumomonyoana, mashindano ya silaha, au upande mmoja kuuzuia mwingine pasipo sababu.”
Ameendelea kusema kuwa "mataifa yaliyojaliwa rasilimali nyingi na mila za pamoja zilizokita mizizi katika mafundisho ya amani ya Kiislamu, lazima yaungane na kutegemea nguvu ya mantiki badala ya mantiki ya nguvu."
Rais mteule wa Iran ameandika kwamba kama hatua ya kwanza, serikali yake "itazihimiza nchi jirani za Kiarabu kushirikiana na kutumia fursa zote za kisiasa na kidiplomasia kuweka kipaumbele katika suala la usitishaji wa kudumu wa mapigano huko Gaza kwa lengo la kusitisha mauaji na kuzuia kupanuka zaidi kwa mzozo huo."Pezeshkian amesema: “Katika muktadha huu, nataka kusisitiza kwamba mataifa yote yanalazimika, chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa 1948, kuchukua hatua za kuzuia mauaji ya kimbari; si kushajiisha mauaji hayo kwa kuanzisha uhusiano na watendaji wake.” Rais mteule wa Iran pia amezipongeza China na Russia kwa kusimama pamoja na Iran "katika nyakati za changamoto" mbalimbali. Pezeshkian ameandika kwamba "Marekani pia inahitaji kutambua ukweli na kuelewa, mara moja na daima, kwamba Iran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo."
342/