Main Title

source : Parstoday
Jumapili

14 Julai 2024

15:40:34
1472039

Iran yamtia mbaroni mhusika mkuu wa shambulio la kigaidi la Kerman

Vikosi vya usalama wa taifa vya Iran vimefanikiwa kumtia mbaroni mmoja wa wahusika wakuu wa miripuko miwili ya kigaidi iliyotokea mwezi Januari mwaka huu katika mji wa Kerman wa kusini mashariki mwa Iran.

Takriban watu 103 waliuawa kidhulma na kigaidi na wengine 211 kujeruhiwa katika miripuko miwili iliyotokea Januari 3, 2024 katika mji wa Kerman, karibu na eneo alipozikwa mmoja wa makamanda wakuu wa kambi ya muqawama yaani Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.

Katika taarifa yake ya jana Jumamosi, Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema kuwa, askari wake wamefanikiwa kumtia mbaroni mmoja wa wapangaji wakuu wa mashambulizi hayo ya kigaidi anayejulikana kwa jina la Abdullah Quetta.Wizara hiyo imeongeza kuwa, taarifa za kijasusi zilizopatikana kutoka kwa Quetta zimekuwa na nafasi kubwa katika kufichua njama nyingi za magenge ya ukufurishaji, zimefichua mambo mengine makubwa yakiwemo maficho ya magaidi katika nchi za ukanda huu. Wizara ya Intelijensia ya Iran mbali na kusema kuwa, kutiwa mbaroni gaidi Quetta ni mafanikio makubwa katika vita dhidi ya ugaidi, lakini imesisitiza kuwa, operesheni za kuwasaka magaidi wengine bado zinaendelea. Katika taarifa hiyo, wizara hiyo imesema kuwa, askari wake wamegundua pia walipo viongozi mbalimbali wa magenge ya kigaidi na wale waliohusika moja kwa moja kwenye vitendo tofauti ya kigaidi humu nchini.

342/