Main Title

source : Parstoday
Jumapili

14 Julai 2024

15:41:56
1472041

BRICS, msingi wa Uhusiano wa Kimkakati kati ya Iran na Russia

Uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) na BRICS umeweka msingi wa kuendelea zaidi uhusiano na ushirikiano wa kistratijia wa Tehran na Moscow.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran na Rais Vladimir Putin wa Russia wamekutana na kujadiliana kandokando ya kikao cha BRICS. Rais wa Russia ameeleza furaha yake juu ya uanachama wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kundi la BRICS na kusema: Ushirikiano wa Iran na Russia na utaendelea kuimarika zaidi.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ameshiriki mkutano huo kwa mwaliko wa Vyacheslav Valodin, Spika wa Bunge la Russia (Duma) na Valentina Matvinko, Mkuu wa Baraza la Shirikisho la Bunge la Russia.

Mwaka jana, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine tatu zilipata uanachama wa BRICS, na sasa jumla ya nchi 9 kutoka mataifa yanayoibukia kiuchumi duniani zimejiunga na kundi hilo. Hili ni mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi ya juu wa Iran kushiriki katika mkutano mkuu wa BRICS baada ya kupata uanachama kamili. Mojawapo ya malengo muhimu zaidi ya ziara ya ujumbe wa Bunge la Iran huko St. Petersburg ni kufuatilia suala la kutumia uwezo wa BRICS katika miamala ya kifedha na kibiashara.

Akizungumzia mkutano wake na Rais Vladimir Putin wa Russia, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Katika mazungumzo na Rais Putin, sambamba na kufuatilia makubaliano ya kifedha ya pande mbili na Mradi wa Coridor, nimesisitiza pia udharura wa kustawisha uhusiano kati ya Iran na Russia. Putin ameeleza imani yake ya kuendelezwa uhusiano kati ya Iran na Russia kama ilivyokuwa katika kipindi cha shahidi Ayatullah Ebrahim Raisi na ameniomba niwasilishe salamu zake za dhati kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei na wananchi wa Iran."

Miongoni mwa madola makubwa, Russia ina historia ndefu zaidi ya uhusiano wa kisiasa na Iran. Wachambuzi wanaamini kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na nafasi muhimu katika siasa za nje za Russia kutokana na eneo lake la kistratijia, kijeopolitiki na kwa kuwa na mambo mbalimbali yanayoipatia nguvu kieneo, na hilo limechangia katika kufanya uhusiano wa pande mbili kuwa wa kistratijia.

Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia ambao umekuwa ukipanuka mara kwa mara katika miongo kadhaa iliyopita, umeshika kasi zaidi katika miaka ya hivi karibuni kwa kuzingatia matakwa ya viongozi wa nchi hizo mbili, na umechora upeo wa wazi wa kupanua zaidi ushirikiano huo mkubwa katika kanda hii.

Masuala ya kieneo na kimataifa, nafasi ya kijografia ya Iran na Russia, haja ya nchi hizo mbili kuwa karibu zaidi kadiri inavyowezekana na umuhimu wa kustawisha uhusiano wa pande mbili vimezidisha kasi katika mchakato wa kustawisha uhusiano wa Tehran na Moscow. Iran na Russia zina maslahi ya pamoja katika ngazi ya kimataifa, kikanda na katika ngazi ya mahusiano ya pande mbili, ambayo yameboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika miaka ya baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti.

Ukweli ni kwamba uhusiano wa pande mbili kati ya Iran na Russia una historia ndefu ya ushirikiano katika masuala yenye maslahi ya pamoja, na kwa sababu hiyo, siasa za Marekani dhidi ya nchi zote mbili zinaongezeka zaidi. Iran na Russia zinapinga juhudi za Marekani za kueneza mfumo wake wa ulimwengu wa kambi moja, na suala la kuunga mkono kuwepo mfumo wa pande kadhaa na kukabiliana na ule wa Marekani ni miongoni mwa mambo yanayotia msukumo katika ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa, kupanuka kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, mbali na kukuza maslahi ya Iran na Russia, kumezinufaisha pia nchi nyingine na kuimarisha amani na usalama wa kieneo na kimataifa.

Kwa mfano, ukaribu na ushirikiano wa Iran na Russia umeimarisha soko la mafuta duniani, na kupelekea kuanzishwa "Opec ya gesi" kwa kushirikiana na baadhi ya nchi nyingine.

Nukta muhimu na ya kuzingatiwa ni kwamba uhusiano na ushirikiano kati ya Iran na Russia umeimarika sana na kuwa na taathira kutokana na mambo na vipengele muhimu, na jambo hilo limeufanya uendelee kuimarika zaidi siku baada ya siku licha ya mabadiliko ya serikali.

342/