Main Title

source : Parstoday
Jumapili

21 Julai 2024

15:43:46
1473547

Iran yapongeza hukumu ya ICJ, yataka kura ya maoni kuamua mustakbali wa Palestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, njia bora zaidi ya kulipatia ufumbuzi suala la Palestina na kukomeshwa jinai za utawala haramu wa Israel, ni kufanyika kura ya maoni itakayowashirikisha Wapalestina wa ardhi zote za taifa hilo ili waamue mustakbali wao.

Nasser Kan'ani amegusia jinsi utawala wa Kizayuni unavyoendelea kupora ardhi za wananchi wa Palestina na kujenga vitongoji haramu vya Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na hukumu ya juzi Ijumaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na kusema kuwa, kutolewa hukumu hiyo dhidi ya Israel ni uthibitisho wa jinsi dunia nzima inavyoguswa na kadhia ya Palestina. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Mauaji ya kimbari, jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita zinazofanywa na utawala wa Kizayuni hususan huko Ghaza ni mambo ambayo yameamsha hisia za walimwengu kutokana na kuona Israel inaendelea kukanyaga haki za wananchi wa Palestina na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Amesema kinachotarajiwa kutoka kwa jamii ya kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kuchukua hatua za kivitendo za kuiadhibu Israel kwa jinai zake na kulisaidia taifa linalodhulumiwa la Palestina liweze kupata haki lilizoporwa kwa makumi ya miaka sasa. 

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi hivi sasa, utawala ghasibu wa Israel unafanya jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina kwa msaada kamili wa nchi za Magharibi hasa Marekani na hakuna Mpalestina yeyote aliyeko salama, si wale wa Ukanda wa Ghaza wala wale wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

342/