Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

22 Julai 2024

16:27:12
1473819

Kiongozi Muadhamu asisitiza juu ya ushirikiano wa bunge na rais kwa ajili ya kuunda serikali inayofaa kiutendaji

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea matumaini yake kuwa kupitia ushirikiano wa Rais Mteule na Bunge, baraza la mawaziri lenye watu waaminifu na wachapakazi litaundwa kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi na wananchi.

Akizungumza siku ya Jumapili katika kikao na Rais Mteule, Spika na wajumbe wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani bunge la Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mafanikio ya rais mteule Massoud Pezeshkia katika nyanja za kiuchumi, kiutamaduni, kimataifa na nyanja nyinginezo ni mafanikio na ushindi wa kila mtu hivyo wote wanapasa kushirikiana na rais mteule katika kufanikisha majukumu yake. Ayatullah Khamenei huku akiorodhesha sifa maalumu za Majlisi katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni za nchi, amezitaka pande mbili za bunge na serikali kushirikiana kwa karibu kwa ajili ya kufikia malengo ya kitaifa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaka bunge lishirikiane na rais mteule katika kuunda baraza jipya la mawaziri katika hali ambayo wawakilishi hao wa bunge ambao ni watungaji wa sheria za nchi katika siku chache zijazo watakuwa na jukumu zito la kupitisha au kuwakataa mawaziri watakaowasilishwa bungeni kwa ajili ya kubuniwa baraza jipya la mawaziri. Kwa ajili hiyo Ayatullah Khamenei amesema kuhusiana na sifa na vigezo vinavyohitajika kwa watu ambao watakuwa mawaziri na wasimamizi wa uchumi, utamaduni, ujenzi na uzalishaji wa nchi, kwamba mawaziri watakaoteuliwa wanapasa kuwa waminifu, wachaMungu na wanaoamini kwa dhati misingi na thamani za Jamhuri ya Kiislamu.Baada ya Kiongozi Muadhamu kumuidhinisha Masoud Pezeshkian kuwa rais wa nchi hapo Jumapili tarehe 28 mwezi huu na kuapishwa bungeni tarehe 30 Julai, Rais atawajibika kuwasilisha majina ya mawaziri wake aliowapendeka bungeni ili kupugiwa kura ya kuwa au kutokuwa na imani nao. Kwa hakika, katika siku zijazo, Bunge si tu litashirikiana na Rais Mteule katika uteuzi wa mawaziri, bali pia litakuwa chombo muhimu zaidi cha kufanya maamuzi katika uteuzi wa mwisho wa mawaziri waliopendekezwa.

Kwa mujibu wa kifungu cha 63 cha Katiba, muda wa kuhudumu wabunge ni miaka minne, ambapo katika kipindi hiki wana jukumu la kutunga sheria ndani ya mipaka iliyoainishwa na katiba na pia wana haki ya kuchunguza na kufuatilia mambo yote ya nchi, ukiwemo utendaji wa serikali.

Kwa hakika, wabunge wana wajibu na majukumu ambayo yameainishwa wazi na sheria katika kuhudumia wananchi. Katika upande wa pili, kama kiongozi nambari mbili nchini baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, rais ana jukumu kubwa kitaifa,  hivyo kuidhinishwa kwa baraza jipya la mawaziri ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa na Bunge. Hio ndio maana Kiongozi Muadhamu akasisitiza sana katika kikao chake cha jana na wabunge wa bunge hilo, kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa taasisi hii na rais mteule, akitilia mkazo kuwa mafanikio ya serikali ni mafanikio ya taifa zima, na kuongeza kuwa taasisi zote zina wajibu wa kushirikiana na serikali katika uwanja huo.

Kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake ya jana, licha ya kuwepo matatizo ya ndani na nje; Iran ina uwezo mkubwa kama vile umoja na mshikamano wa kitaifa, na ili kufikia malengo ya juu na kutatua matatizo ya wananchi, ushirikiano wa dhati na wa karibu unahitajika kuwepo kati ya bunge na serikali ili kuwezesha kutatuliwa matatizo ya nchi katika sekta mbalimbali.