Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

22 Julai 2024

16:27:40
1473820

Pezeshkian: Wanaoiwekea vikwazo Iran waliwapa maadui silaha za kemikali

Rais mteule wa Iran ameyakosoa vikali madola ambayo yameiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu akisisitiza kuwa, mataifa hayo yana historia nyeusi kwa kupeana silaha zilizotumiwa dhidi ya taifa hili katika miaka ya 1980.

Masoud Pezeshkian, Rais mteule wa Iran amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa: Wanaotekeleza vikwazo dhidi ya wananchi wa Iran kwa kutumia visingizio hewa, ndio wale wale waliokuwa wakiwapa silaha maadui wa nchi hii.

Dakta Pezeshkian amesema hayo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mashambulizi ya silaha za kemikali dhidi ya kijiji cha Zardeh, mkoa wa magharibi wa Kermanshah, yaliyofanywa na wanajeshi vamizi wa Iraq mnamo Julai 1988.

Kwa akali wakazi 275 wa kijiji hicho waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 1,400 walidhurika kwa gesi ya sumu na kupata maradhi ya aina mbalimbali kufuatia mashambulizi hayo ya mabomu ya kemikali.Rais mteule wa Iran amesisitiza kuwa, watenda jinai waliotoa silaha za kemikali zitumike dhidi ya taifa la Iran wanapaswa kushtakiwa mara moja katika mahakama za kimataifa.

Nchi zilizousheheneza utawala wa dikteta wa Iraq, Saddam Hussein kwa silaha za kemikali wakati huo ni pamoja na Marekani, Ujerumani (Magharibi), Uholanzi, Uingereza na Ufaransa.

Hivi karibuni pia, Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema katika siku ya kumbukumbu ya mashambulizi ya silaha za kemikali katika mji wa Sardasht nchini Iran kwamba: Wale waliounga mkono jinai za utawala wa Saddam Hussein dhidi ya watu wa Sardasht nchini Iran, hivi sasa wanaunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza. 



342/