Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

22 Julai 2024

16:28:50
1473822

Kukabidhiwa madaraka serikali ya awamu ya 14 kwa njia ya amani na utulivu kamili

Kukabidhiwa madaraka rais mpya wa Iran, ni moja ya dalili za wazi za mkondo wa kukabidhi madaraka kwa njia ya amani na utulivu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran, jambo ambalo linachukuliwa kuwa mfano mzuri na wa kuigwa na hata na nchi zinazodai kutekeleza demokrasia.

Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tangu siku ya kwanza baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais, serikali iliyoko madarakani huwajibika kushirikiana na rais mteule kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kukabidhi uongozi wa serikali kwa rais mpya.

Kuhusu suala hili, serikali ya awamu ya 13 pia imetoa ushirikiano mkubwa wa kuhamisha habari na kufafanua hali ya sasa kwa timu ya Daktari Masoud Pezeshkian, Rais Mteule wa Iran.

Katika duru ya pili ya uchaguzi wa awamu ya 14 ya rais ambayo ilifanyika tarehe 5 Julai mwaka huu, Masoud Pezeshkian alichaguliwa kuwa rais wa tisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya hafla ya kuidhinishwa na kuapishwa kuwa rais, Pezeshkian atawajibika kuwaarifisha mawaziri wake ili wapate kupigiwa kura ya kuwa na imani nao bungeni.

Kama walivyofanyiwa marais wengine wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Pezeshkian ataapishwa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) tarehe 30 Julai baada ya kuidhinishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hafla ya kuidhinishwa Rais Mteule wa Iran, itafanyika siku ya Jumapili tarehe 28 Julai mbele ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mchakato wa kukabidhiwa madaraka kwa serikali mpya, baada ya kuthibitishwa usahihi wa uchaguzi na Baraza la Walinzi wa Katiba, hati ya uhalali na utambulisho wa rais hutumwa katika Ofisi ya Kiongozi Muadhamu.

Hati hiyo ni waraka unaothibitisha usahihi wa mchakato wa uchaguzi wa urais na usahihi wa rais aliyechaguliwa. Waraka huo hutaja jina la rais aliyechaguliwa na idadi ya kura alizopata.

Kwa mujibu wa ibara ya 9 ya kifungu cha 110 cha katiba, kumuidhinisha rais kabla ya sherehe ya kuapishwa kwake bungeni na baada ya kuchaguliwa kwa kura za wananchi ni moja ya majukumu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Kwa kutilia maanani kuwa kuidhinishwa rais ni moja ya majukumu ya Kiongozi Muadhamu kwa mujibu wa katiba, hivyo suala hilo si la kimaonyesho hata tu, bali madamu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hajamuidhinisha rais, rais huwa hana uhalali wowote wa kuongoza serikali.

Uidhinishaji wa rais pia una maana ya kusimamia kazi zake wakati wa urais na ikiwa atakengeuka kutokana na kanuni na misingi iliyowekwa, anaweza kuondolewa mamlakani wakati wowote. Kwa mujibu wa Ibara ya 10, kipengele cha 110 cha Katiba, hatua ya mwisho ya kuondolewa rasmi madarakani rais huchukuliwa na Kiongozi Muadhamu, hatua ambayo hutekelezwa baada ya bunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye na kisha uamuzi huo wa bunge kutiwa saini na Mahakama ya Juu nchini.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 1 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, muhula wa urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa miaka minne na huanza tangu tarehe ya uidhinishaji unaofanywa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Hatua inayofuata baada ya uidhinishaji huo ni kuapishwa rais, ambapo hufika bungeni na kula kiapo mbele ya wajumbe wa Baraza la Walinzi wa Katiba, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama na maafisa wengine wa kijeshi na kitaifa, kwa mujibu wa Ibara ya 121 ya Katiba.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, rais aliyechaguliwa hula kiapo cha kutumia uwezo na umahiri wake wote katika kutekeleza majukumu aliyopewa na hatimaye kusaini kiapo hicho.

Katika sherehe ya kuapishwa rais, mbali na Spika na wabunge wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, baadhi ya viongozi na shakhsia kutoka ndani na nje nchi pia hualikwa kuhudhulia hafla hiyo ya kuapishwa rais.

Baada ya hafla hiyo na kwa mujibu wa kanuni za ndani za bunge, rais ana wiki mbili za kuwasilisha mpango wake na pia majina ya mawaziri wake ambapo bunge huwa na muda wa wiki moja baada ya hapo kuwachunguza katika kamisheni za kitaalamu za bunge na kisha kuwapigia kura ya kuwa au kutokuwa na imani nao.

342/