Main Title

source : Parstoday
Jumanne

23 Julai 2024

19:22:57
1474077

Iran yavunja ukiritimba katika bidhaa za nyuklia

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Iran imeweza kuvunja ukiritimba katika sekta ya nyuklia huku bidhaa na huduma zake zilizoundwa nchini hivi leo zikiuzwa katika soko la kimataifa.

Mohammad Eslami ameyasema hayo katika mahojiano na tovuti ya Khamenei.ir, ambayo yalichapishwa siku ya Jumatatu. Ameendelea kusema kwamba: "Uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika teknolojia ya nyuklia umevunja ukiritimba katika sekta hii, ili huduma na bidhaa zetu ziwepo katika masoko ya dunia, na baadhi zikiuzwa nje ya nchi kadhaa."

Eslami pia amebainisha kuwa Iran ina uwezo wa kusafirisha dawa za kinyuklia katika nchi mbalimbali na kuongeza kuwa, Iran pia inauza nje maji mazito ya nyuklia.

Watafiti wa Iran wamefaulu kuzalisha isotopu thabiti ambazo ni za kimkakati, za gharama kubwa, na za ubora wa juu.

Aidha amesema Iran imepokea maombi ya ushirikiano baada ya kufanya Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia na kushirikisha nchi 22 mwezi Mei.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imesajili mafanikio mengi katika mpango wake wa amani wa nishati ya nyuklia pamoja na kuwepo vikwazo vya Marekani na nchi nyingine za Magharibi.

Ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizotia saini Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Nyuklia (NPT), Iran pia imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

342/