Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Syria (SANA); Rais Assad jana Jumatatu alitembelewa na Ali Asghar Khaji, mshauri mkuu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala maalumu ya kisiasa pamoja na ujumbe aliofuatana nao, ambapo katika mazungumzo na ujumbe huo alitilia mkazo kuimarishwa zaidi uhusiano na kuimarishwa ushirikiano na uratibu baina ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga mbalimbali.
Katika kikao hicho mshauri mkuu wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala maalumu ya kisiasa amezungumzia masuala mbalimbali hususan uhusiano wa pande mbili katika nyuga tofauti.Ali Asghar Khaji, pia alikutana na Faisal Al-Maqdad, Waziri wa Mambo ya Nje na wa masuala ya Wahajiri wa Syria na kuzungumzia uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais wa Syria, hivi karibuni alifanya mazungumzo ya simu na Daktari Masoud Pezeshkian, Rais mteule wa Iran na kumtakia mafanikio na heshima katika kutekeleza jukumu hilo kubwa na muhimu la kitaifa, na akasema, Iran ni taifa lenye historia kongwe na ing'aayo na lenye mafanikio makubwa; na Iran ni nchi yenye nguvu na akaongeza kwa kusema: uhusiano kati ya Tehran na Damascus ni imara mno na msingi wake ni kusaidiana na kuungana mkono pande mbili katika nyakati ngumu.
Bashar Assad ameulezea pia uhusiano baina ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni msingi wa uthabiti na sababu kuu ya kuzuia eneo hili lisibebeshwe ubeberu wa maajinabi na akasema: kwa kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, watafanya jitihada za kuimarisha na kuufanya madhubuti zaidi uhusiano huo baina ya pande mbili.
342/