Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

26 Julai 2024

17:07:51
1474558

Kiongozi Muadhamu: Uungaji mkono wa ulimwengu kwa Palestina unatokana na moyo wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema harakati zinazofanywa duniani siku hizi kwa manufaa ya Palestina ni matokeo ya moyo wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha habari cha Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, matamshi hayo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyotolewa katika kikao na washiriki wa Kongamano la Mashahidi wa mkoa wa Tehran, kilichofanyika tarehe 15 Mei yalisambazwa Alhamisi jioni kwenye ukumbi wa kongamano hilo katika Haram Tukufu ya Imam Khomeini (MA).

Katika mkutano huo, Ayatullah Khamenei alibaini kuwa miongoni mwa baraka za mujahidina katika zama za Kujihami Kutakatifu (vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran) ilikuwa ni kufikisha ujumbe wa istiqama na muqawama ndani na nje ya mipaka ya nchi. Ameongeza kuwa: "Wataalamu wengi wanatangaza kwa uwazi kwamba harakati zinazofanyika duniani  siku hizi  kwa manufaa ya Palestina zinatokana na roho ya mapinduzi ya Kiislamu. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongeza kuwa: "Nara na misimamo tunayoishuhudia hii leo ya kuunga mkono Palestina duniani kote ni ile ile misimamo ya Imam Khomeini (RA) na  wananchi wa Iran."

Akiashiria harakati za wanachuo na wahadhiri wa vyuo vikuu nchini Marekani katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, Ayatullah Khamenei  amesema uungaji mkono huo ni kielelezo cha baraka za harakati ya taifa la Iran na msukumo kutoka kwa Imam Khomeini,  jambo ambalo ni la kipekee katika historia ya zama hizi.

Halikadhalika amesema  uungaji mkono wa wanachuo na wahadhiri wa Marekani kwa Palestina umeenea kiasi kwamba serikali ya Marekani katika kukabiliana na hali hiyo inakiuka nara zake zote (za eti kutetea haki za binadamu) na kuwatumia polisi kuwakandamiza na kuwakamata wanafunzi na maprofesa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameeleza kuwa, moyo na hamasa ya vijana wa Iran katika miaka ya hivi karibuni ya kushiriki katika nyuga kama makabiliano na magaidi wa Daesh au utawala wa Kizayuni inatokana na moyo huo huo wa kipindi cha Kujihami Kutakatifu na akasema: "Katika matukio ya kivita, fitna za miaka ya nyuma, ikiwemo fitna ya mwaka 2009 mjini Tehran, vijana ambao hawakumuona Imam wala hawakushuhudia zama za Kujihami Kutakatifu, waliingia katika medani wakiwa na ari na azma  ya zama hizo na kukwamisha mpango wa adui wa kuleta matatizo kwa ajili ya nchi na wananchi."

342/