Matamshi hayo ya Balozi Amir Said Iravani yamekuja kufuatia kuuawa shahidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Haniyeh na mlinzi wake mmoja waliuawa shahidi usiku wa kuamkia jana Jumatano mjini Tehran baada ya eneo walilofikia kupigwa na kitu. Haniyeh alikuwepo hapa Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais wa 14 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Daktari Masoud Pezeshkian.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa jana Jumatano alimwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama pamoja na Katibu Mkuu wa umoja huo akiwaambia kuwa, jinai ya kutisha iliyofanywa na Israel dhidi ya mgeni rasmi na wa ngazi za juu ndani ya ardhi ya Iran, ni uvunjaji mkubwa wa haki ya kujitawala Jamhuri ya Kiislamu na ni uvunjaji wa wazi wa sheria zote za kimataifa, hivyo Iran nayo ina haki zote za kujibu vikali jinai hiyo ya Wazayuni.Vile vile amesema kuwa, kwa kuzingatia matokeo mabaya sana yatakayosababishwa na jinai za Israel dhidi ya amani na usalama wa ukanda huu mzima, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilaani vikali mashambulizi ya kigaidi ya Israel na kutoheshimu kwake haki ya kujitawala ardhi nzima ya Iran, kama ambavyo linapaswa kulaani pia jinai za Israel katika ardhi za Lebanon na Syria.
342/