Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

3 Agosti 2024

16:31:24
1476352

Baada ya UN, Iran yaitaarifu EU: Tutalitia adabu genge la wahalifu la utawala wa Kizayuni wa Israel

Iran itatumia haki yake ya asili na halali ya kuliadhibu "genge la wahalifu la Kizayuni" kwa shambulio lake la kigaidi la siku ya Jumatano iliyopita, ambalo lilipelekea kuuawa mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) Ismail Haniyeh mjini Tehran.

Haya yamesemwa na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Baqeri Kani, katika mazungumzo yake ya simu na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell. 

Baqeri amesisitiza kuwa, kitendo cha kigaidi cha utawala ghasibu wa Israel mbali na kukiuka mipaka ya ardhi na mamlaka ya kitaifa ya Iran, kimehatarisha amani na usalama wa kieneo na kimataifa. 

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezikosoa baadhi ya nchi za Ulaya kwa kushirikiana na Marekani kuzuia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani mauaji ya kigaidi ya Haniyeh wakati wa kikao chake cha dharura siku ya Jumatano. 

Baqeri amesisitiza kuwa, misimamo ya madola hayo inayoiunga mkono Israel, inayodhihirika katika kimya chao kuhusiana na uchochezi wa Wazayuni huko Yemen na Lebanon, imeupa moyo utawala huo ghasibu wa kuendeleza vitendo vyake vya kichokozi na hivyo kuhatarisha amani na usalama wa kikanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amekiri kuwa Iran ina haki halali ya kutetea mipaka na mamlaka yake na ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mivutano na uwezekano wa kutokea vita kamili katika eneo la Magharibi mwa Asia na matokeo yake mabaya.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Hamas, Ismail Haniyeh, ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, aliuawa pamoja na mlinzi wake katika shambulio la Israel kwenye makazi yake siku ya Jumatano.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameuambia utawala wa Israel ujitayarishe kwa "jibu kali" kwa mauaji ya Haniyeh na kueleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inapaswa kulipiza kisasi cha damu ya kiongozi huyo wa mapambano ya Palestina.

342/