Ujumbe wa Mfalme wa Saudia kwa Rais wa Iran umekabidhiwa kwa Rais Pezeshkian mjini Tehran na Mwanamfalme Mansour bin Mutaib Al Saud Waziri Mshauri wa Serikali na Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Saudi Arabia ambaye pia ni mshauri wa Mfalme Salman.
Mwanamfame Mansour amemfikishia Rais wa Iran salamu kutoka kwa Mfalme Salman, Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, na Mkuu wa Baraza la Mawaziri na kueleza matarajio yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Iran.
Katika ujumbe wake huo, Mfalme Salman amemtakia afya njema na ufanisi Rais wa Iran, maendeleo na ustawi wa taifa na wananchi wa Iran, na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu. Mfalme wa Saudi Arabia pia amesisitiza udharura wa kustawisha uhusiano kati ya nchi na mataifa mawili ndugu na kuendelea kuwasiliana na kushauriana ili kuimarisha amani na usalama wa kikanda na kimataifa.
Rais wa Iran pia ameshukuru kwa ujumbe na upendo ulioonyeshwa na Mfalme wa Saudia na Mwanamfalme wa nchi hiyo na kusema: Mazungumzo kati yake na Mwanamfalme wa Saudia yalikuwa na manufaa na kwamba uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia, mbali na kutilia maanani suala la kuwa jirani na kuwa na uhusiano wa kindugu, unafungamana pia na maingiliano na kidini na kiitikadi na kutufanya kuwa kitu kimoja.
Rais wa Iran ameeleza kuwa maadui na wale wanaoyatakia mabaya mataifa haya mawili wanajaribu kila wawezalo kuibua hitilafu kati ya nchi mbili ili kufanikisha malengo yao haramu. Rais Masoud Pezeshkian ameongeza kuwa: Iran na Saudi Arabia ni lazima zisambatishe njama hizo kwa umakini, umoja na mshikamano.
Iran na Saudi Arabia, mwezi Juni na Agosti mwaka jana zilianzisha tena mahusiano ya kidiplomasia katika miji mikuu ya nchi mbilii. Ali Reza Inayati Balozi mpya wa Iran nchini Saudi Arabia aliwasili Riyadh mwezi Septemba mwaka jana, na siku hiyo hiyo Abdullah bin Saud Al-Enezi balozi mpya wa Saudia nchini Iran alianza kutekeleza majukumu yake ya kidiplomasia mjini Tehran. Kuhuishwa uhusiano wa pande mbili kati ya Iran na Saudia na kupunguza mivutano katika eneo hili la Magharibi mwa Asia kumekuwa na manufaa kwa nchi zote mbili. Nchi zote mbili zimetoa kipaumbele kwa mipango ya maendeleo na zimeandaa ramani ya muda mrefu katika uwanja huo; jambo ambalo ufanikishaji wake unahitaji kudumishwa amani na utulivu.
Kwa kuzingatia mtazamo huu, kuhuishwa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia kumeipatia Riyadh fursa mbalimbali ili kupata amani na utulivu unaohitajika kufanikisha malengo yake ya ndani ya maendeleo. Dira ya 2030 ya Mpango Mkuu wa Saudia wa kuibadili nchi hiyo na kuwa nchi yenye uchumi usiotegemea mafuta, inahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta zisizo za mafuta kama utalii, lojistiki, bandari, burudani na ulinzi.
Aidha baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kushindwa kuiburuta Saudi Arabia katika Makubaliano ya Abraham (The Abraham Accords) umeanzisha vita vya pande zote dhidi ya Gaza na kuathiri eneo zima la Magharibi mwa Asia. Hii leo imewabainikia watu wote kuwa Netanyahu na serikali yake ya mrengo wa kulia inayopinga amani, inajaribu kusalia mamlakani kinyume cha sheria huku ikiendeleza vita na hali ya mchafukoge na kuchochea kwa makusudi vitendo vya kigaidi.
Kuendelea jinai za Israel huko Gaza katika kipindi cha miezi 10 iliyopita na taathira zake huko Lebanon, Yemen, katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, kumeliweka eneo la Mashariki ya Kati katika hatari nyingi.
Rais Shahid Ebrahim Raisi na Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Waziri Mkuu wa Saudia walifanya mazungumzo yao ya kwanza ya simu tangu kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi mbili katika siku ya nne tu baada ya kuanza vita dhidi ya Gaza. Katika mazungumzo hayo, pande hizo zilikubaliana kuhusu kusitishwa jinai za kivita dhidi ya Palestina na kukuza umoja wenye nguvu wa Kiislamu. Novemba 11 mwaka jana pia Shahid Raisi alifanya ziara mjini Riyadh kwa lengo la kuhutubia Mkutano wa Dharura wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuhusu Gaza.
342/