Bunge la Kenya hivi sasa linaendelea kuwahoji wale waliopendekezwa kuhudumu katika baraza jipya la mawaziri la Kenya baada ya lile lililokuwepo kuvunjwa kufuatia maandamano ya wananchi.
Dakta Martin Kimani, mwakilishi wa kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa mjini New York hadi Aprili mwaka huu, amesema Marekani haina ustahiki wa kutoa maagizo kuhusu utawala bora.
Amesema kauli ya Marekani ya kutoa maagizo kuhusu utawala bora kwa wengine ni mbinu inayotumiwa na Washington kupotosha fikra za umma duniani kutokana kushindwa kwake katika uga wa kimataifa. Ametoa mfano na kusema Marekani imefeli kimataifa katika kadhia ya vita vya sasa vya Israel dhidi ya Gaza kwani imeshindwa kushinikiza usitishaji vita. Tangu Oktoba mwaka jana utawala katili wa Israel, kwa himaya ya Marekani, umekuwa ukiendeleza vita vya mauaji ya umati dhidi ya Gaza ambapo hadi sasa utawala huo umeua Wapalestina karibu arubaini elfu.
Balozi Kimani pia amesema Marekani haina ustahiki wa kutoa maagizo kwa nchi zingine kuhusu utawala bora wakati yenyewe inakumbwa na ghasia za kisiasa, kuporomoka imani katika taasisi zake za uchaguzi na wasi wasi kuhusu kukabidhiana madaraka baada ya uchaguzi wa rais nchini humo mwezi Novemba.
Ameongeza kuwa "Marekani inapaswa kuacha kutoa maagizo kwa nchi zingine, kisha ifanye marekabisho mapya katika mfumo wake wa demokrasia na ihakikishe kuwa kuna usitishwaji vita huko Gaza".
Chanzo: parstoday