"Utawala wa Kizayuni umezaliwa katika ugaidi, na haumiliki kitu chochote kinachounda taifa," Meja Jenerali Hossein Salami amesema hayo leo katika hafla iliyofanyika mjini Tehran kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Waandishi wa Habari.
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba Israel itapata jibu la uhakika kwa mauaji ya Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), akiwa mjini Tehran.
Amesema kwamba "Israeli itakapopokea kipigo katika sehemu na wakati mwafaka, na wakati huo itatambua kuwa ilifanya makosa katika mahesabu yake."
Kamanda Salami amezungumzia jinsi utawala huo ghasibuulivyoundwa katika eneo la Asia Magharibi mwaka 1948 ambako kulifuatiwa na kufukuzwa mamia ya maelfu ya Wapalestina katika makazi yao katika vita vilivyoungwa mkono na nchi za Magharibi.
Salami amefananisha vitendo vya mauaji ya mara kwa mara vya utawala wa Israel na "kimbunga cha moto" ambacho kimeuzunguka utawala huo.
"Ukatili huu, ni mashimo ambayo Waisraeli wamejichimbia wenyewe, na watajizika polepole," amesema Meja Jenerali Hossein Salami na kuongeza kuwa, "Mara tu watakapopata jibu kali, wataelewa kuwa wamefanya makosa mengine."
Matamshi hayo yanaashiria yale yaliyotolewa na Ayatullah Sayyid Ali Khamenei baada ya mauaji ya Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Hamas) kuhusu "majibu makali" dhidi ya ukatili huo na akasisitiza wajibu wa Jamhuri ya Kiislamu wa kulipiza kisasi damu ya kiongozi huyo wa Hamas.
342/