Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

5 Agosti 2024

16:43:01
1476798

Pezeshkian: Kosa 'kubwa' la Israel la kumuua kigaidi Haniyah litajibiwa

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kumuua kigaidi Ismail Haniyah, Kiongozi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ni 'kosa kubwa' ambalo halitapita hivi hivi bila kupewa majibu.

Dakta Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake na Ayman Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan ambaye yuko ziarani hapa Tehran na kuongeza kuwa, mauaji hayo ya kigaidi ya Haniyah yamekanyaga sheria na kanuni zote za kimataifa.

Rais wa Iran ameeleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu inatazamia nchi zote za Kiislamu na mataifa huru duniani yatalaani jinai za namna hii. Amesisitiza kuwa, maadui wakubwa na wavunjaji wa uhuru, demokrasia na haki za binadamu wanatumia uwezo wao wa kisayansi na kioperesheni kufanya vitendo vya kigaidi na jinai za kihaini.

"Wanadai kutetea uhuru, demokrasia na haki za binadamu lakini wanamuarifisha yeyote ambaye anajiepusha kuwafuata kuwa adui wa kanuni na maadili hayo," ameeleza Rais wa Iran.

Kwingineko katika matamshi yake, Rais Pezeshkian amesema sera ya mambo ya nje ya serikali yake itazingatia kukuza amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi na duniani kwa ujumla.

Amesisitiza ulazima wa kuimarishwa ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu ili kukomesha ukatili na jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan kwa upande wake, amesema Amman inalaani mauaji ya Haniyah ambayo anasema ni sehemu ya juhudi za Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu za kueneza na kushadidisha mivutano katika eneo.

342/