Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo leo katika mazungumzo yake ya kila wiki na waandishi wa habari na sambamba na kulaani jinai ya Israel ya kumuua shahidi kidhulma Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, vitendo kama hivyo vya kigaidi si tu havitii doa katika nia ya kweli ya taifa imara la wanamuqawama la Palestina, lakini pia vinazidi kulitia nguvu katika mapambano yao dhidi ya utawala wa Kizayuni na kwa ajili ya ukombozi wa Quds Tukufu. Amesema, jinai ya utawala wa Kizayuni ya kumuua kiwoga na kidhulma kiongozi wa ngazi za juu wa kisiasa wa taifa la Palestina hapa Tehran imefanyika katika hali ambayo kiongozi huyo alikuwa mgeni rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jinai hiyo ni uvunjaji wa wazi kabisa wa haki na sheria za kimataifa, na ni kwenda kinyume na maadili ya kisiasa yanayohesahimiwa na jamii nzima ya kimataifa. Dunia inapaswa kuunga mkono kutiwa adabu utawala dhalimu wa Israel.
Vile vile Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran imeitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kuitisha kikao cha dharura mjini Jeddah Saudi Arabia suala ambalo limekubaliwa na wanachama wote. Kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC kinatarajiwa kufanyika tarehe 7 Agosti mwaka huu.
342/