Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

8 Agosti 2024

15:08:26
1477380

Iran: Utawala wa Kizayuni utaweza kudhibitiwa tu kwa kuchukuliwa hatua kali dhidi yake

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, utawala wa Kizayuni mtenda jinai utaweza kudhibitiwa iwapo tu kutachukuliwa hatua kali dhidi yake na kulazimishwa kwa nguvu kuheshimu sheria za kimataifa.

Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo leo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, lau kama jamii ya kimataifa ingetekeleza vizuri majukumu yake, leo hii tusingelishuhudia miezi 10 wa jinai, ukatili, maangamizi ya kizazi na mauaji ya halaiki ya wanawake na watoto wadogo yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza. 

Ameandika hayo kujibu matamshi ya kijuba na kifidhuli ya waziri wa fedha wa utawala wa Kizayuni aliyedai kuwa watawaua kwa njaa Wapalesitna milioni 2 katika mkabala wa kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni waliko mikononi mwa harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, dunia inapaswa kuelewa kuwa, genge la wahalifu na watenda jinai linaloongozwa na Benjamin Netanyahu ndani ya serikali ya utawala wa Kizayuni litaendelea kukaidi kuheshimu sheria za kimataifa maadamu hakutachukuliwa hatua kali za kivitendo za kutiwa adabu Israel na kulazimishwa iheshimu sheria hizo.

Amesema, matamshi ya kiburi ya waziri wa fedha wa Israel kuhusu kuwaua kwa njaa Wapalestina milioni 2 yanakinzana kikamilifu na maadili, ubinadamu na sheria zote za kimataifa lakini hachukuliwi hatua zozote. Ameziambia nchi za Ulaya kwamba matamshi yenu ya kulaani tu ufidhuli huo wa Wazayuni hayatoshi, ni bora kuweka maneno pembeni na kuchukua hatua za kivitendo za kukata uhusiano wa kisiasa na kijeshi na Israel.

342/