Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

12 Agosti 2024

14:53:17
1478217

China yatangaza kuunga mkono Iran katika kulinda usalama wake

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi anasema Beijing inaiunga mkono Iran katika kutetea "mamlaka yake, usalama na heshima ya taifa" huku Tehran ikiahidi kuiadhibu vikali Israel kutokana na mauaji ya Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Hamas.

Katika mazungumzo ya simu na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani Jumapili, Wang alisisitiza kwa mara nyingine msimamo wa  Beijing wa kulaani mauaji ya mkuu wa Hamas jijini Tehran mwishoni mwa mwezi uliopita.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema katika taarifa yake kwamba, wakati wa mazungumzo hayo Wang Yi  amesema shambulizi lililopelekea kuuawa  Haniyeh limekiuka mamlaka ya kujitawala ya Iran na kuwa tishio kwa uthabiti wa eneo hilo.

Aliongeza kuwa mauaji ya Haniyeh "yamedhoofisha moja kwa moja mchakato wa mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza na kudhoofisha amani na utulivu wa kikanda."

Haniyeh aliuawa Julai 31, alipokuwa Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.

Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema mauaji ya Haniyeh yalipangwa na kutekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa msaada wa serikali ya Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei ameuonya utawala wa Israel kuhusu "jibu kali" kwa mauaji ya Haniyeh na kusema kuwa ni jukumu la Jamhuri ya Kiislamu kulipiza kisasi damu ya kiongozi huyo wa mapambano ya kupigania ukkombozi wa Palestina.

342/