Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

2 Septemba 2024

16:24:40
1482423

Hali mbaya ya hewa, ukungu ndio chanzo kikuu cha ajali ya helikopta ya Rais Raisi, ripoti ya mwisho yasema

Uchunguzi wa mwisho wa Jeshi la Iran kuhusu ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha Rais Ebrahim Raisi na wenzake kadhaa mwezi Mei mwaka huu unasema tukio hilo lilisababishwa na hali mbaya ya hewa iliyojumuisha ukungu mkubwa.

Helikopta iliyokuwa imembeba Rais Ebrahim Raisi (63), waziri wa zamani wa mambo ya nje, Hossein Amir-Abdollahian, na watu wengine sita ilianguka Mei 19 kwenye mlima uliofunikwa na ukungu kaskazini magharibi mwa Iran. Miili yao ilipatikana siku moja baadaye baada ya juhudi kubwa za timu za waokoaji.

Ripoti iliyochapishwa na Mkuu wa Jeshi la Iran jioni ya jana Jumapili, imekanusha uwezekano wa kufanyika hujuma au uharifu kama sababu ya tukio hilo la kusikitisha, ikisema "hali tata ya hewa, na anga ya eneo la tukio katika msimu wa machipuo ndio sababu kuu ya ajali hiyo.Imeongeza kuwa "kuibuka kwa ghafla wingu kubwa la ukungu mnene" kulisababisha helikopta hiyo kuanguka kwenye mlima.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nyaraka zote zinazohusiana na ukarabati na matengenezo ya helikopta hiyo tangu iliponunuliwa na kutumika kabla ya tukio hilo zilipitiwa kwa kina na wataalamu wa kijeshi na kiraia, ambao walitangaza kuwa hatua zote zimefanyika chini ya kanuni za kawaida.

Ripoti hiyo iimesema kuwa wataalamu pia wamechunguza njia ya helikopta na kuthibitisha kuwa ilifuata njia yake iliyoainishwa mapema na haikuwa na mkengeuko wakati wa safari.

Uchunguzi huo pia umekanusha uwezekano wa kitendo chochote cha hujuma ya sehemu na mifumo ya helikopta iliyoanguka. Pia imekanusha dhana kwamba huenda helikopta hiyo ililengwa na mifumo ya hujuma, mashambulizi ya mtandaoni au maeneo ya sumaku na leza.


342/