Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ireland, Micheál Martin ambapo akiashiria uungaji mkono wa Iran kwa juhudi zinazoendelea za kusimamisha vita huko Gaza, amesema kuwa, Tehran inaunga mkono makubaliano yoyote ya makundi ya muqawama na wananchi wa Palestina.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran pia amesema kuwa, Tehran itaunga mkono makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yatakayokubaliwa na Wapalestina na Harakati ya Muqawama wa Kiiislamu wa Palestina (HAMAS).
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, jamii ya kimataifa lazima ichukue hatua za "haraka na madhubuti" za kukomesha jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza.
Araghchi ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuondolewa hali ya wasiwasi katika eneo hili, lakini utawala wa Kizayuni unalenga kueneza ghasia na kuzieneza katika maeneo mengine ukiwemo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kwa upande wake Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ireland akielezea wasiwasi wake juu ya kuenea kwa hali ya wasiwasi katika eneo la Asia Magharibi amesema kuwa, nchi yake inataka kusitishwa mara moja kwa vita huko Gaza na kubadilishana mateka sambamba na kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza haraka iwezekanavyo.
Zaidi ya watu 40,000 wa Gaza wameuawa shahidi na takriban laki moja kujeruhiwa katika mashambulizi ya Wazayuni huko Gaza ambapo asilimia 70 kati yao ni wanawake na watoto. Kulingana na ripoti za kimataifa, mauaji ya Wapalestina huko Gaza ni aina mbaya zaidi ya mauaji ya kimbari na ya watoto wachanga kuwahi kufanywa katika historia ya mwanadamu.