Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

6 Septemba 2024

18:02:16
1483261

Iran yakanusha madai ya Marekani ya kuingilia uchaguzi wa nchi hiyo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha madai ya Mwanasheria Mkuu wa Marekani aliyedai kuwa eti Tehran inangilia uchaguzi wa nchi hiyo na kusema kuwa, kwa mara nyingine tena, tunakanusha madai yanarudiwarudiwa ya eti tunaingilia uchaguzi wa Marekani.

Nasser Kan'ani amenukuliwa na shirika la habari la Mehr  akisema hayo na kuongeza kuwa, kwa mara nyingine tunasema kuwa, madai hayo yanayorudiwa mara kwa mara hayana msingi wowote na yanatolewa kwa chuki na malengo maalumu ya kujinufaisha kisiasa ndani ya Marekani. Tunapinga kikamilifu madai hayo.

Amesema, wakuu wa Marekani hawawezi kurekebisha mambo waliyoyaharibu ikiwa ni pamoja na mapengo na matatizo mengi ya ndani ya Marekani, kwani migogoro hiyo ina mizizi mirefu ya kimuundo, kisiasa na kijamii. Hivyo kuropoka na kutoa tuhuma dhidi ya mataifa mengine nje ya mipaka ya Marekani, hakuwezi kuwasaidia viongozi wa Marekani kutatua matatizo yao chungu unzima ya ndani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, serikali ya Marekani ambayo ni kiranja wa kuingilia kinyume cha sheria masuala ya nchi nyingine duniani hususan nchi huru na ina rodha ndefu ya vitendo vyake hivyo vya kibeberu na kuharibu amani na usalama wa mataifa mengine, haina haki ya kuzituhumu nchi nyingine tena bila ya ushahidi wowote. Viongozi wa Marekani wabebe wenyewe madhara na mzigo wa migogoro yao ya ndani, wasizibebeshe nchi nyingine matatizo yao na wasijaribu kuficha vitendo vyao viovu nyuma ya mgongo wa kuzituhumu nchi nyingine.


342/