Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

6 Septemba 2024

18:03:20
1483263

Iran yalaani hatua ya Marekani ya kuiba ndege ya Rais wa Venezuela

Msemaji Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani hatua ya serikali ya Marekani kukamata ndege inayotumiwa na rais wa Venezuela.

Nasser Kan'ani sambamba na kulaani hatua hiyo amesema kuwa, kitendo hicho ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Msemaji Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya ulazima wa kuheshimiwa sheria na kanuni za kimataifa na kubainisha kwamba, kitendo hicho cha Marekani kinakiuka wazi sheria na mikataba ya kimataifa.

Hivi majuzi Marekani iliiteka ndege hiyo katika Jamhuri ya Dominica, ikidai kuwa eti upatikanaji wake umekwenda kinyume na vikwazo vya Marekani. 

Serikali ya Caracas imesema: "Marekani imeiba ndege ambayo imekuwa ikitumiwa na Rais wa nchi yetu kwa madai ya kukiukwa vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Venezuela na ambavyo ni kinyume cha sheria zote duniani."

Vyombo vya habari vimeripoti taarifa iliyotolewa na Idara ya Mahakama ya Marekani ikitangaza kuwa, Washington imeteka ndege iliyokuwa inatumiwa na Rais Nicolas Maduro wa Venezuela katika ardhi ya Dominican, hatua ambayo Venezuela imesema ni uharamia wa kiserikali na imeapa kulipiza kisasi.

Serikali ya Venezuela imeilaani vikali Washington kwa kitendo chake cha kuiteka ndege ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na kukitaja kitendo hicho kuwa ni muendelezo wa uharamia na uhalifu wa Marekani.

342/*