Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

6 Septemba 2024

18:04:21
1483266

HAMAS yaitaka Marekani iulazimishe utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeitaka Marekani iulazimishe utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake katika ukanda wa Ghaza na usikwamishe juhudi za kimataifa za kusitishwa jinai hizo.

Televisheni ya Al Jazeera imenukuu taarifa ya HAMAS ikisema kuwa, inaitaka Marekani iuweke utawala wa Kizayuni chini ya mashinikizo makubwa ili ukomeshe jinai zake dhidi ya watu wasio na hatia huko Ghaza. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Khalil al-Hayya, Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya HAMAS yenye makao yake nchini Qatar amesema katika taarifa hiyo kwamba, kama kweli Marekani na hasa rais mwenyewe wa nchi hiyo, Joe Biden, wana nia ya kweli ya kufikia makubaliano ya kusimamisha vita na kubadilisha mateka, basi hawana budi ila kuuwekea utawala wa Kizayuni mashinikizo makubwa ya kuulazimisha ukomeshe jinai zake na waache kuiunga mkono Israel kama vipofu wasioweza kuona upande wowote. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, HAMAS bado inaunga mkono mpango wa amani uliopendekezwa na Biden na yale yaliomo kwenye muswada wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa. 

Taarifa hiyo ya HAMAS pia imesema: Sisi bado tumeshikamana na Azimio nambari 2735 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka. 

Katika sehemu yake ya mwisho, tamko hilo la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS inasema: Tunaonya kuhusu hatari ya kutumbukia kwenye mtego wa Netanyahu wa kurefusha muda wa mazungumzo kwa shabaha ya kupata muda zaidi wa kufanya jinai zake za kinyama dhidi ya Wapalestina.

342/