Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

6 Septemba 2024

18:05:26
1483269

Kiongozi wa Ansarullah akosoa tawala za Kiarabu kwa kunyamazia kimya jinai za Israel, kuvunjiwa heshima Qur'ani

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen amezikosoa baadhi ya tawala za Kiarabu kwa kukaa kimya huku utawala ghasibu wa Israel ukiendelea na ukatili wake dhidi ya Wapalestina na kukivunjia heshima kitabu kitukufu cha Kiislamu cha Qur'ani katika Ukanda wa Gaza.

Abdul-Malik Badruldeen al-Houthi ameyasema hayo katika hotuba ya televisheni iliyotangazwa kutoka mji mkuu wa Yemen Sana’a siku ya Alhamisi mchana. Ameongeza kuwa: "Nchi za Kiarabu zinatazama tu jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, mashambulizi ya kuchomwa moto misikiti na kuvunjiwa heshima nakala za Qur'ani Tukufu bila ya kuwa na misimamo ya wazi kuhusiana na suala hilo."

Al-Houthi amesisitiza umuhimu wa wote katika ulimwengu wa Kiislamu kuwa na roho ya kujitahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu, yaani Jihadi, huku akionya kwamba Waislamu watapoteza heshima na uhuru wao ikiwa watapuuza suala hilo muhimu.

Kiongozi huyo wa Ansarullah ameendelea kusema kuwa: "Baadhi ya tawala za nchi za Kiarabu zinajaribu kumtuliza adui Mzayuni na kufikia mapatano naye ili kujilinda". Ameziona tawala hizo za Kiarabu kwamba hataka kama zitajipendekeza kwa adui, hatimaye zitatupiliwa mbali pindi zitakapokuwa hazitakiwi tena.

Mkuu wa Ansarullah ameendelea kuwapongeza wapiganaji wa muqawama wa Palestina walioko Gaza kwa kupambana na vikosi vya kijeshi vya Israel kwa silaha zisizo za kisasa na kusema: “Hata majeshi makubwa ya baadhi ya nchi za Kiarabu hayakuweza kustahimili mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni kwa kiasi kikubwa kama walivyofanya wapiganaji wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Amesisitiza kuwa wananchi wa Gaza wanastahimili mashambulizi ya kikatili ya Israel na vita vya mauaji ya halaiki, ambavyo vimeamsha dhamiri ya binadamu hata katika nchi zisizo za Kiislamu.

Kwingineko katika matamshi yake, Kiongozi wa Ansarullah ameashiria operesheni za kijeshi za baharini za Yemen dhidi ya meli za kibiashara zenye mafungamano na utawala haramu wa Israel na kusema operesheni hizo zinafanyika kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Amesisitiza kuwa, maadui wamekiri kushindwa kwao kusimamisha operesheni hizo za kijeshi za kulipiza kisasi katika Bahari Nyekundu na nje ya Bahari Nyekundu.

342/