Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limetangaza katika taarifa yake kuwa, Meja Jenerali Tamir Yadai, kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya jeshi hilo, amejiuzulu wadhifa wake huo kwa sababu za kibinafsi. Vyombo vya habari vya Kizayuni hapo awali vilitangaza kuwa kulikuwepo na uwezekano wa Jenerali Yadai kuchukua nafasi ya Mkuu wa Majeshi Jeshi la Israel. Habari za kujiuzulu kamanda huyo wa jeshi katili la Israel zimekuja katika hali ambayo taarifa zinasema idadi ya wanajeshi wa Kizayuni waliojeruhiwa katika vita vya Gaza ni zaidi ya 10,000.
Tofauti za mitazamo kati ya viongozi wa utawala haramu wa Israel zimezidi kupamba moto, huku mawaziri wa zamani wa baraza la mawaziri la Netanyahu wakimtuhumu kuwa hawezi kusimamia vita vya Gaza.
Benny Gantz na Gadi Eisenkot, makamanda wawili wa zamani jeshini ambao pia waliwahi kuwa mawaziri katika baraza la mawaziri la Netanyahu, wameonya katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kwamba: "Israel iko katika hali mbaya zaidi tangu kuanzishwa kwake, na haijafikia malengo yoyote ya vita hivyo." Akiwajibu Gantz na Eisenkot, Netanyahu amewaambia: "Acheni kuingilia masuala ya vita vya Gaza." Naye Avigdor Lieberman, Waziri wa zamani wa Vita wa utawala wa Kizayuni pia amekosoa siasa za Netanyahu na kuzitaja tabia zake kuwa za kutowajibika.
Viongozi hao wa Kizayuni wanataka makubaliano yafikiwe haraka na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, kuhusu kuachiliwa kwa wafungwa wa Kizayuni. Hata hivyo Netanyahu, ambaye anapaswa kushtakiwa kwa kesi mbalimbali za rushwa baada ya vita, anazuia makubaliano yoyote kufikiwa kuhusu suala hili.
Sambamba na maandamano ya familia za mateka wa Kizayuni, migomo imekuwa ikifanyika kwa kiasi kikubwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel.
Migomo hiyo imefanyika sambamba na maandamano makubwa ya kushikamana na familia za mateka wa Kizayuni huko Gaza na kupinga kitendo cha Benjamin Netanyahu cha kuzuia makubaliano ya kubadilishana mateka. Kumefanyika pia migomo katika uwanja wa ndege wa Ben-Gurion, idara ya usafiri wa umma na vituo vya vyombo vya kiuchumi vya utawala wa Kizayuni.
Netanyahu amekabiliwa na migogoro mingi ya ndani katika siku za hivi karibuni, na kutokana na kuendelea kwa vita vya Gaza, yeye na baraza lake la mawaziri hawana uwezo wa kushughulikia malalamiko ya Wazayuni. Vigogo katika utawala wa Kizayuni wa Isarel wanakiri kwa usahihi kwamba hali katika utawala huo haijawahi kuwa mbaya kama ilivyo hivi sasa huku kukiwa na migomo na maandamano ya mara kwa mara.
Wapizani ndani ya utawala haramu wa Israel pia wanamtuhumu Netanyahu kwamba anakwamisha kwa makusudi mapatano na Hamas kuhusu usitishaji vita huko Gaza ili serikali yake iendelee kubakia madarakani. Kimsingi kuendelea vita Gaza ni kwa maslahi ya Netanyahu kwa sasa.
Baada ya kuanza operesheni ya wanamuqawama au wapigania ukombozi wa Palestina ya Kimbunga cha Al Aqsa mnamo Oktoba 7 2023, utawala wa Kizayuni ulidhani kwamba vita vyake vya kikatili dhidi ya Gaza vingemalizika haraka. Hata hivyo utawala huo umeshtushwa na uwezo mkubwa wa kivita wa harakati za muqawama za Palestina
Hivi sasa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel halijafanikisha malengo yake yoyote katika Ukanda wa Gaza pamoja na kuwa linapata uungaji mkono mkubwa wa Marekani na madola mengine ya Magharibi.
Hali mbaya leo ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni matokeo ya uchochezi wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni katika eneo; lakini mara hii utayarifu na kusimama kidete makundi ya muqawama kumesambaratisha njama za Wazayuni na kupelekea kuzuka mgogoro mkubwa na endelevu katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu.
342/