Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

7 Septemba 2024

16:02:32
1483515

Wananchi wa Algeria wanapiga kura leo katika uchaguzi wa rais

Wananchi wa Algeria waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanaelekea katika masanduku ya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua Rais.

Raia wa Algeria wanapiga katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kumuongezea muhula mwingine wa miaka mitano madarakani rais Abdelmadjid Tebboune.

Zaidi ya Waalgeria 800,000 wanaoishi nje ya nchi tayari walianza kupiga kura.

Rais Tebboune, mwenye umri wa miaka 78, anapewa nafasi kubwa ya kumshinda mgombea mwenye msimamo wa wastani Abdelaali Hassani na mgombea wa kisoshalisti Youcef Aouchiche katika kinyang'anyiro cha kuongoza nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Changamoto kubwa inayomkabili kiongozi huyo ni kuongeza idadi ya wapiga kura watakaojitokeza, baada ya kushinda mwaka 2019 kwa asilimia 58 ya kura.Idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza 2019 ilifuatia maandamano ya kuunga mkono demokrasia ya Hirak, ambayo yalimuondoa rais wa zamani Abdelaziz Bouteflika kabla ya kukomeshwa na polisi. Mamia ya waandamanaji walitiwa nguvuni.

Uchaguzi wa leo wa Algeria unafanyika miezi mitatu kabla ya muda uliokuwa umepangwa hapo awali.

 Uamuzi wa kufanya uchaguzi wa mapema wa urais tarehe 7 Septemba mwaka huu ulifikiwa kufuatia mkutano ulioongozwa na Rais wa nchi hiyo Abdelmadjid Tebboune na kuhudhuriwa na wabunge na mkuu wa majeshi.

Rais Tebboune ambaye atatimiza miaka 79 ifikapo mwezi Novemba, alichaguliwa kushika hatamu za uongozi mwezi Disemba mwaka 2019 baada ya maandamano ya waungaji mkono wa demokrasia mwezi Februari mwaka huo ambayo yalimlazimisha Rais aliyekuwa madarakani kwa muda mrefu huko Algeria, Abdelaziz Bouteflika, kujiuzulu.


342/