Amir Saeed Iravani amesema hayo katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Majaribio ya Nyuklia na kubainisha kuwa, kuadhimisha siku hiyo ni fursa kwa Jamii ya Kimataifa ya kuulazimisha utawala wa Israel ujiunge bila ya masharti yoyote na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT) na kuviweka vituo vyake vyote vya nyuklia chini ya usimamizi kamili wa Wakala wa Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).
Iravani ameongeza kuwa, hali ya sasa inatia wasiwasi, kwa sababu utawala wa Israel unazitishia nchi za eneo kwa maangamizi ya kinyuklia; na maghala ya silaha zake za nyuklia ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa moja ya nchi zilizotia saini mkataba wa kukabiliana na majaribio ya nyuklia CTBT, inauchukulia mkataba huo kuwa hatua moja mbele kuelekea katika utokomezaji wa silaha za nyuklia; na kuhusiana na suala hilo inaitakidi kwamba, mkataba wa CTBT hauwezi kuchukua nafasi ya utokomezaji kamili wa silaha za nyuklia, kwa hivyo, utokomezaji wa silaha za nyuklia inapasa uendelee kuwa kipaumbele kikuu cha Jamii ya Kimataifa; na aina zote za majaribio ya nyuklia inapasa zipigwe marufuku kikamilifu.
342/