Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

7 Septemba 2024

16:05:13
1483521

Idadi ya vifo Ghaza yapindukia 40,900 baada ya jeshi la Israel kuua Wapalestina wengine 61

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limewaua shahidi Wapalestina wengine 61 katika mashambulizi kwenye Ukanda wa Ghaza, na kuongeza idadi ya vifo kufikia 40,939 tangu Oktoba 7, 2023. Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Afya ya Ghaza.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Wapalestina wasiopungua 94,616 wamejeruhiwa pia kutokana na mashambulio ya kinyama na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel dhidi ya Ghaza. "Vikosi vya Israel vimeua watu 61 na kujeruhi wengine 162 katika 'mauaji' manne dhidi ya familia katika saa 48 zilizopita," imebainisha taarifa ya Wizara ya Afya ya Ghaza na kuongezea kwa kusema: "watu wengi wangali wamenasa chini ya vifusi na barabarani kwa sababu waokoaji hawawezi kuwafikia". Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS Oktoba 7, 2023.Jeshi la Kizayuni linaendeleza mashambulio dhidi ya maeneo mbalimbali ya Ghaza licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja mapigano katika ukanda huo uliowekewa mzingiro.

 Vizuizi vinavyoendelea kuwekwa na jeshi la Israel dhidi ya Ghaza vimesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, na kuacha sehemu kubwa ya eneo hilo kuwa magofu. Utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa pia na tuhuma za mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ambayo imeamuru kusitishwa operesheni za kijeshi za utawala huo katika mji wa kusini wa Rafah, ambapo zaidi ya Wapalestina milioni moja walikuwa wamepatiwa hifadhi kabla ya eneo hilo kuvamiwa Mei 6.../


342/