Victor Aguayo, mkuu wa mpango wa chakula wa UNICEF amesema kuwa, watoto hawa huko Gaza wanaugua utapiamlo mkali na wanahitaji matibabu ya haraka.
UNICEF inaripoti kuwa watoto 9 kati ya 10 huko Gaza hawapati vitamini za kutosha kwa ajili ya ukuaji, na ongezeko kubwa la wastani wa utapiamlo kati ya watoto na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha katika Ukanda wa Gaza ni mambo ambayo yameyafanya maisha yao kuwa hatarini.
Wakati huo huo Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa la (UNICEF) lilisema wiki iliyopita kwamba, zoezi la kutoa chanjo ya polio kwa watoto wa Kipalestina katika eneo la Ukanda wa Gaza lilikuwa miongoni mwa kampeni ngumu na hatari zaidi duniani licha ya kusitishwa kwa muda mapigano katika eneo hilo kwa ajili ya zoezi hilo.
UNICEF imesema kwamba Gaza, iliyoharibiwa na vita vya miezi 11 vya Israel, "tayari ni mahali hatari zaidi duniani kuwa mtoto, na licha ya kusitishwa mashambulizi ya Israel kwa ajili ya chanjo ya polio, kampeni ya kutoa chanjo inakabiliwa na hatari kubwa na vikwazo visivyoweza kufikirika, ikiwa ni pamoja na barabara zilizoharibika na kubomolewa miundombinu ya afya, watu waliokimbia makazi yao, uporaji na kuvurugwa njia za usambazaji.
342/