Mbobezi wa sheria duniani, Mohamed Chande Othman, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Ujumbe huo Huru wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli kuhusu yanayoendelea Sudan amewaeleza waaandishi wa habari mjini Geneva kwamba, "tangu katikati ya Aprili mwaka 2023, mzozo wa Sudan umeenea hadi majimbo 14 kati ya 18 na kuathiri nchi nzima na ukanda huo, na kuwafanya Wasudan milioni nane kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mzozo huo, na zaidi ya milioni mbili kulazimishwa kukimbilia nchi jirani.”Katika ripoti yao hiyo ya kwanza tangu Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilipounda jopo hilo mwaka jana 2023, wajumbe wa jopo hilo wamesisitiza kwamba pande zote mbili zinazohasimiana, yaani wanajeshi wa Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya wanamgambo vya Usaidizi wa Haraka (RSF), pamoja na washirika wao, wanahusika na mashambulizi makubwa, ya kiholela na ya moja kwa moja yaliyohusisha mashambulizi ya anga na makombora dhidi ya raia, skuli, hospitali, mitandao ya mawasiliano na miundombinu mingine muhimu ya maji na umeme ikionesha kutozingatia kabisa ulinzi wa wasio wapiganaji.
Joy Ngozi Ezeilo, mmoja wa wajumbe wa jopo hilo la wataalamu huru ameeleza kwamba, waathirika walisimulia kushambuliwa wakiwa kwenye nyumba zao na kutishiwa kifo au kuumizwa kwa ndugu au watoto wao kabla ya kubakwa na zaidi ya mtu mmoja.”
Wachunguzi hao mbali na kupendekeza uwekaji zaidi wa vikwazo vya silaha kwa Sudan, wamehimiza pia kianzishwe kikosi cha kimataifa cha kulinda amani kitakachotumwa nchini Sudan kikiwa ama chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa au mamlaka nyingine ya kikanda.../
342/