Main Title

source : Abna
Jumapili

8 Septemba 2024

07:14:01
1483629

Indhari ya Jordan kuhusu njama ya Israel ya kuyahudisha maeneo ya Kiislamu na Kikristo mjini Al-Quds

Wizara ya Wakfu ya Jordan imetahadharisha kuhusu kushadidi hatua za utawala wa Kizayuni zenye lengo la kueneza Uyahudi katika maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo katika mji mtakatifu wa al-Quds (Jerusalem).

Wizara hiyo imetoa wito kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kutimiza wajibu wao kuhusu mji huo mtakatifu.

Imesema mataifa ya Kiarabu na Kiislamu yanapaswa kutoa shinikizo kwa utawala wa Israel na kuzuia majaribio yake ya kutaka kuudhibiti Msikiti wa Al-Aqsa ulioko mjini al Quds, tovuti ya al-Mashhad al-Arabi imeripoti.

Wizara hiyo imeitaja hali ya sasa ya al-Quds kuwa ni hatua hatari katika majaribio ya kubadilisha hadhi ya kihistoria na kisheria ya maeneo ya Kiislamu na Kikristo ya mji huo.

Kabla ya hapo, Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Jordan, Mohammad Khalaileh alikashifu kukithiri na ukiukwaji wa hadhi ya Msikiti wa Al-Aqsa unaofanywa na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na walowezi wa Kizayuni wenye itikadi kali wanaopata himaya ya serikali.

Ameonya juu ya madhara ya uvamizi huo na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa kwa waumini wa Kiislamu wanaofika katika Msikiti wa Al-Aqsa.

Khalaileh amesisitiza kwamba Waislamu wana haki za kidini, kihistoria na kisheria kwa Msikiti wa Al-Aqsa, akiongeza kuwa msikiti huo ni eneo la Kiislamu pekee, na majaribio yoyote ya kugawanya au kudhibiti eneo hilo takatifu hayakubaliki.

chanzo: parstoday