Main Title

source : Abna
Jumapili

8 Septemba 2024

14:19:28
1483715

Mazungumzo ya ABNA na kuhani mpya wa Kikristo wa Kiislamu:

Ninahesabu wakati mmoja wa kutokea kwa Hadhrat Mahdi (a.t.f.s) na Hadhrat Masih(a.s)

Padri wa Kikristo na mpya katika Kiislamu: Ukweli ni kwamba siku zote nimekuwa na wasiwasi juu ya kukua na kupanuka kwa Uislamu, na ninahesabu dakika sawa za kudhihiri kwa Mtume wetu Isa (amani iwe juu yake), pamoja na Imam wetu Hadhrat Mahdi (amani iwe juu yake).

Somo la leo la Shirika la Habari la ABNA ni kuhusiana na Muislamu mpya wa Brazil. Alikuwa mfuasi wa Ukristo / (au) Mfuasi wa Hadhrat Issa (a.s), na alitumikia watu wa Brazili kama kuhani wa Kikristo.

Katika yafuatayo, ni mahojiano ya kuvutia ya ripota wa Shirika la Habari la Ahlul_Bayt (a.s) na Mwanazuoni huyu wa Brazil:

Al_Salam Alaikum.

Tunatanguliza shukrani kwako kwa kutupa wakati wako, na tafadhali tunaomba ujitambulishe.

Assalamu Alaikum.

Jina langu ni "Renato", nilikuwa kuhani Mkristo ambaye niliingia katika neema ya Uislamu. Kwa sasa ninaishi Sergipe, Brazil.

Tafadhali tuambie jinsi ulivyosilimu na uliifahamuje Familia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?. Au kwa maneno mengine ni nini kilitokea hadi ukavutiwa na Madhehebu ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao)?.

Kama nilivyosema mimi mwanzoni nilikuwa Mchungaji (Kuhani) na nilikubali Uislamu kwa elimu na maarifa ya Biblia, baada ya hapo nilikutana na mtu aitwaye "Mayubi" na kupitia vitabu alivyonijulisha (au alivyoviarifisha kwangu) niliifahamu Familia ya Mtume (Amani iwe juu yao).

Ilikuwa ni maarifa ya kuvutia sana kwangu mimi nilipotambua na kufahamu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s) pia alichagua Mrithi (Kiongozi baadae yake) ; Kwa sababu desturi hii siku zote imekuwa miongoni mwa Mitume wote ambapo walikuwa wakiwachagua Mawasii wao, kama vile Nabii Musa na Nabii Isa (Amani iwe juu yao), na pia Mtume wa Uislamu akamchagua Hadhrat Ali bin Abi Talib (Amani iwe juu yake) ili aufikishe Uislamu kwa wengine na Ulimwengu mzima Wasio ujua Uislamu wapate kuujua.

Himidi zote ni zake Mwenyezi Mungu, kuona kwamba umeweza kuipitia njia ya Ukristo mpaka Uislamu kwa salama, ni sababu gani kuu ya mwelekeo wako kuelekea Shule ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), na katika njia hii, ni matamu yepi na matatizo gani uliyoyapitia?.

Nilipokuwa Kuhani, kila mara nilijaribu kuketi na kutafuta ukweli, na nikaupata Uislamu kwa njia hii, na kwa kupitia njia hii, niliifikia Familia ya Mtume, na leo hii nina furaha kubwa kwamba hatimaye nimeufikia ukweli na uhakika. Ama kuhusu nukta uliyoisema, ndiyo, niliona (nilikumbana na) matatizo na manyanyaso mengi tu; kwa sababu hiyo ni asili (au ni kawaida) ya kazi; kwani si ni kweli kwamba hata Manabii na Mawasii wao walikumbana na dhulma na manyanyaso?!. Lakini kwa nimeweza kuufikia Uislamu, kwangu Mimi hayo ndio matamu (mazuri ya kheri) niliyoyapata. Sisi tunapaswa kuzoea haya mambo. Tunapaswa kuvumilia vita na Mitihani, kisha baada ya hilo tusubirie Ushindi, kwa nini?! Ni kwa sababu Qur'an Tukufu inasema: "Nusra ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Ushindi wa karibu".

Je! ni kwa kiwango gani Wanafunzi Wahubiri / Mubalighina wa Kidini walikuwa na ufanisi katika kufahamiana kwako na Uislamu?.

Kama unataka ukweli wa hili, ni kwa kiwango kikubwa sana! Kwanza, Mubalighina / Wahubiri fulani walipokuja katika eneo letu, nilijaribu kufanya urafiki nao, na nilipokewa kwa itikio chanya na la upendo; hata niliwaalika kwa siku moja ili urafiki wetu uzidi kuimarika, na leo nina furaha kwamba baada ya muda mrefu, urafiki wangu na ndugu Waislamu wa Iran umedumishwa, na ninaomba kwamba Mwenyezi Mungu aifanye kuwa nyepesi njia ya Dini kwa ajili yetu sisi sote, iwe hivyo kwa Mashia na pia kwa ndugu zetu Masunni.

Bila shaka unajua kwamba sambamba na kutunza Imani (Itikadi) zetu, ni lazima tuishi kwa amani na watu wa Dini zingine na Madhehebu nyinginezo. Kwa maoni yako, ni vipi Wahubiri wa Kidini katika nchi kama Brazil wanaweza kuhifadhi Dini na Imani yao na kuwaalika watu wengine kwenye Shule ya Uislamu na kufuata familia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Amani iwe juu yao) bila kuingia katika aina yoyote ile ya mvutano na migogoro?

Ili kujibu swali lako, nadhani kuna jambo muhimu la kuzingatia.

Jambo kuu na la msingi ni kwamba: Watu wa Brazil wanapenda hivyo kuwa ikiwa mtu atazungumzia Uislamu, basi habari zake kwa Wafuasi wa Ukristo ziwe zinatosha. Ikiwa Mwanafunzi au Mhubiri anayekuja Brazil kuhubiri Dini hana habari (maarifa) kuhusu Biblia na Ukristo, hilo humfanya mtu mwingine (anayesikikiza) ahisi kwamba anashughulika na mtu ambaye hajasoma.

Kwa hiyo, kwa kuzingatia kwamba idadi kubwa ya watu wa Misikiti mingi nchini Brazil ni wahamiaji, ni muhimu kwa Wahubiri wetu wapendwa kuongeza habari zao (Maarifa yao) kuhusu mambo ya kawaida ya Uislamu na Ukristo, na kuwa na majibu yanayofaa kwa mashaka / shubuhati za Wakristo; Njia hii, kwa upande mmoja, inaimarisha mijadala ya Kidini miongoni mwa Waislamu wahamiaji, na kwa upande mwingine, tunaweza kuwaalika (kuwaita) Wabrazil wengi zaidi kwenye Uislamu.

*Pia umekutana na Ayatollah Ramezani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), wasikilizaji wetu wa mahojiano haya wanaweza kupendezwa na ufafanuzi wako kwamba ni jinsi gani ulivyomuona, yeye ni binadamu wa namna gani?.

Kwa maoni yangu, Ayatollah Ramezani, ni mtu wa kiroho sana, mtu wa kimaanawi na Mcha-Mungu, ambaye pia ana elimu na fadhila.

Ninaomba Mwenyezi Mungu amlinde daima na ninatumai atarejea tena Brazil.

*Mwisho kabisa, tunashukuru kwa uwepo wako katika mahojiano na mazungumzo haya, ikiwa una nukta au mapendekezo yoyote, tafadhali zungumza.

Hapana, sina nukta maalum. Pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mwaliko nilioupata wa kuwa hapa, ambao umenifanya niwafahamu zaidi ndugu zangu Waislamu wa Iran na shughuli za Uhubiri / Tabligh. Ukweli ni kwamba siku zote nimekuwa nikihofia kukua na kuenea kwa Uislamu na ninahesabu dakika sawa za kudhihiri kwa Mtume wetu Isa (amani iwe juu yake) pamoja na Imam wetu, Hadhrat Mahdi (a.t.f.s).

Ninakushukuru kwa kuandaa ripoti hii, na ninakuombea Dua njema.

*Sisi katika Shirika la Habari la ABNA, pia tunakushukuru tena na tena, na tunakutakia mafanikio katika hatua zote za maisha yako.