Kula kila tunda kwa msimu wake, kula matunda yaliyoiva, kuosha matunda kabla ya kula na kutupa matunda ambayo yameoza (na kuharibika) kiasi, ni miongoni mwa mapendekezo ya kuvutia mno ya Maasumina (a.s) kuhusiana na matunda (na umuhimu wake).
Shirika la Habari la Ahlul_Bayt (a.s) / ABNA: Uislamu ni Dini pana ambayo inatilia maanani nyanja zote za maisha ya Mwanadamu. Pia (Uislamu) unajali kuhusu riziki ya Mwanadamu na pia ufufuo wa Mwanadamu. Baadhi ya mapendekezo ya Uislamu si wajibu au si haramu, lakini ni bora kuyazingatia ili kuwa na maisha bora na yenye afya. Sayansi (Elimu) ambazo Wanadamu huzipata kupitia uzoefu na majaribio; wakati mwingine zinaenda sambamba na kuafikiana na ukweli na uhakika, na wakati mwingine zinaenda kinyume na ukweli na uhakika.
Mara nyingi katika Historia, tumeona kwamba dhana za Kisayansi zilizothibitishwa na Wanasayansi zinakataliwa au kukamilishwa na Wanasayansi wengine baada ya miaka michache.
Hii ndiyo sifa ya Mwanadamu ambaye ana uwezo mdogo na hawezi kuelewa vipimo vyote vya uumbaji kwa juhudi zake zote.
Hatujui Mwanasayansi yeyote anayesema kwamba anajua kila kitu au anayesema kwamba leo hii Sayansi (Elimu) imegundua kila kitu kinachowezekana, na kwamba hakuna kitu kilichoachwa na ambacho hakijulikani kwa Mwanadamu. Bali ni kinyume chake, kadiri tunavyosonga mbele ndivyo tunavyozidi kugundua kuwa kuna mengi zaidi ambayo Wanadamu bado hawayajui.
Lakini Sayansi ambayo ina asili ya ufunuo, kwa vile inatoka kwenye asili ya uumbaji, haina makosa kwa njia yoyote ile. Ingawa Wanadamu wanaweza wasielewe pembe zake zote, hii haiondoi ukweli na uhakika wake.
UISLAMU NA USHAURI WA KIAFYA
Kwa vile lishe na afya ni sehemu ya maisha ya Mwanadamu, Uislamu haughafiliki na hilo na umetoa mapendekezo. Ingawa, kutoa mapendekezo haya, kukusanya na kuainisha katika sura ya sayansi ya kina, kuchukua msaada kutoka kwa mafanikio ya majaribio ya leo ili kuyaelezea na kuyaelewa, na pia kutofautisha baina ya masimulizi sahihi na simulizi za uwongo katika uwanja huu; ni kazi ngumu na inayotumia na inahitaji wakati na muda mrefu, na inahitajia ujuzi na sayansi mbalimbali za Hadithi na zisizo za Hadithi.
Pia ifahamike kwamba sehemu kubwa ya sayansi hizi hazijatufikia, au fikra ya kuzikubali haikuwepo wakati wa Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao). Lakini kwa hali yoyote ile, maelfu ya simulizi kuhusu lishe na afya sasa ziko mikononi mwetu.
Katika Qur'an Tukufu na mila za Kiislamu, majina ya idadi kubwa ya matunda na vyakula yametajwa.
Hasa kwa kuzingatia kuwa yametajwa katika Hadithi / Riwaya zao mahsusi. Inapaswa kusemwa kwamba matunda, baraka hizi nzuri za Mwenyezi Mungu, sio mahsusi (au sio) kwa ajili ya maisha haya ya Duniani tu, na Qur'ani Tukufu inawaahidi watu wa Peponi na hii:
"Na kwa ajili yao matunda ya namna yoyote watakayochagua, na nyama ya ndege waipendayo"[1].
Kwa maana kwamba: Pembeni ya matunda, watakula nyama pia.
Kuna mapendekezo mengi kuhusu matumizi ya matunda katika vitabu vya Hadithi, na tunataja machache sehemu kama mfano:
SHIFAA / UPONYAJI KATIKA MATUNDA YALIYOIVA
Matunda yanapaswa kuliwa baada ya kuiva - katika rangi nyekundu au njano - na yakiwa ya kijani na mabichi, haipaswi kuchumwa. Kwa sababu katika hali hiyo ni hatari, na wakati mwingine kuyala (katika hali hiyo) kunaweza kusababisha tatizo la kusahau na kuwa na kumbukumbu dhaifu.
Hata tafsiri ya riwaya hiyo inasema kwamba: Matunda yanapoliwa yakiwa yameiva, huwa kuna uponyaji ndani yake, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'an Tukufu:
«کُلُوا مِن ثَمرِه إذا أثمَرَ»
"Kila matunda ya Bustani yatakapoiva, kuleni katika matunda yake"[2][3].
KULA KILA TUNDA MWANZONI MWA MSIMU WAKE, NA KULIEPUKA MWISHONI MWA MSIMU HUO
Lazima utakuwa na uzoefu kwamba matunda ya msimu wa kwanza yana ladha tofauti. Ikiwa hayatakabiliana na hila za ajabu za Wanadamu kuyafanya yaive mapema kabla ya wakati wake, yanakuwa na faida sana. Mtume Mtukufu (s.a.w.w) anasema:
«علیکم بالفاکِهةِ فی إقبالِها؛ فإنّها مَصَحَّةٌ للأبدانِ مَطرَدَةٌ للأحزانِ، و ألقُوها فی إدبارِها، فإنّها داءُ الأبدانِ».
"Ni juu yenu kula Matunda yanapoiva katika msimu wake; kwani yanakuwa ni afya kwa miili yenu, na yanaondoa huzuni (ni pumziko la huzuni), na achaneni nayo unapoisha msimu wake, kwa sababu yanakuwa ni chanzo cha maumivu ya miili yenu" [4].
Ikiwa umewahi kugundua na kuzingatia, baadhi ya matunda mwishoni mwa msimu wake hayana ladha ya asili na uchangamfu kama ule wa mwanzo wa msimu wake, na yana ladha ya matunda yaliyooza na yaliyoharibika.
Bila shaka, kuna aina tofauti za Makomamanga. Kuna aina kadhaa za Makomamanga katika nchi yetu ya Iran, na baadhi ya aina fulani ya Makomamanga hayo yana ladha zaidi na ni yenye faida zaidi kuliko aina nyinginezo. Huenda hatujawahi kuiona aina hiyo (ya Makomamanga yenye ladha zaidi) hapo awali, lakini wanasema kuwa kuna aina ya Komamanga ambayo inajulikana kama aina isiyokuwa na mbegu, na ina ubora wa juu sana na yenye ladha zaidi.
TUMIA (KULA) MATUNDA YOTE KATIKA MSIMU WAKE
Imam Sadiq (Amani iwe juu yake) alimwambia Mufadhal bin Omar katika muktadha huu kuwa:
Tazama jinsi baadhi ya mimea (na miti) inavyotumiwa kwa wakati fulani, ni kama vile [baadhi yao] huzaa matunda wakati wa joto, ili watu waiendee kwa shauku zaidi; na lau wakati wa matunda haya [ya majira ya joto] ungekuwa ni katika msimu wa baridi, watu wasingekuwa na hamu ya kuyavuna, pamoja na ukweli huu kwamba rangi ya matunda hayo ingebadilika na pia yangedhuru mwili (wa Binadamu); kwani huoni kwamba wakati mwingine matango huiva wakati wa baridi na watu huepuka kuyavuna na kuyala?, kama vile ambavyo kuna watu ambao (wao) hawaepuki kula vitu vyenye madhara na visivyoendana na matumbo yao [5] ; Mwenyezi Mungu amepanga (misimu) majira na matunda ya kila majira kwa namna ambayo kila majira huleta (matunda) chakula kinachohitajika kwa majira hayo.
Mazao na mboga za kila msimu zinaweza kufidia ukosefu (upungufu) wa msimu uliopita, lakini siku hizi, kutokana na maendeleo yaliyopatikana katika kilimo, kuna matunda mengi katika kila msimu. Kwa mfano, katika msimu wa baridi, tunakabiliwa na kila aina ya magonjwa ya virusi, ambayo tunahitaji kula kwa wingi vyakula vyenye Vitamini C kwa wingi, na matunda yote ya msimu huu, kama vile Machungwa, Tangerines (Machenza), Mandimu (Mandimu: Ni Matunda ya manjano ya ‘ellipsoidal’ ya mti ambayo hutumika Ulimwenguni kote kwa ajili ya upishi na na wakati mwingine hutumiwa kwa matumizi yasiyokuwa ya upishi), nk, yana uwezo mkubwa wa kuzalisha (kutoa) Vitamini C (Tanbihi: Mboga za majani na matunda ya uchachu na yenye rangi ya njano hutoa kwa wingi Vitamin C, lakini pia tunaweza kupata Vitamini C kwa wingi kwa kula Maini, Maziwa na Mayai). Pia, msimu wa majira ya joto, wakati (ambao) mwili huhitaji maji zaidi, umejaa matunda mengi ya juisi.
Katika msimu wa chemchemi (The Spring Season), kwa dalili kwamba kiwango cha mboga za majani na matunda mapya kinakuwa ni kidogo mno mwishoni mwa majira ya joto, inashauriwa kuhifadhi (kuweka benki ya) vyakula vya vitamin ili kutoa vitamin vilivyopotea mwilini (wakati wa majira ya joto), na kisha kula kwa wingi mboga za majani na matunda katika msimu wa chemchemi (spring). Tikiti Maji (Watermelon) kwa sababu ya hali ya joto na muundo wake ulivyo, linafaa kwa msimu wa joto, na matumizi yake (yaani: Kula Tikiti Maji) wakati wa msimu wa baridi ni hatari (kwa afya yako). Hapo zamani za kale, Wairan walitumia (walikuwa wakila) Maboga (Malenge) kwenye Shab-e- Cheleh (Yalda Festival au The Night of the Fortieth: Tanbihi: Katika tamasha la Yalda au Shab-e- Cheleh au Usiku wa Arobaini), Wairan husherehekea kuwasili kwa majira ya baridi, kufanywa upya kwa jua na ushindi wa mwanga dhidi ya giza).
Kwa kuwa mwili wa Mwanadamu unahitaji aina mbalimbali za vyakula katika hali tofauti za kila mwaka, Mwenyezi Mungu pia ameumba asili (nature) kwa namna ambayo inaweza kutosheleza mahitaji yake. Hebu tusibadili mpangilio wa asili (nature) kwa matakwa yetu. Huenda msiamini kuosha matunda kabla ya kuyala, lakini huko nyuma, ingawa watu hawakutumia sumu ya kemikali kama leo, Ahlul-Bayt (Amani iwe juu yao) - walishauri na - waliamuru kwamba matunda yaoshwe kwanza kabla ya kuliwa. Kwa mujibu wa riwaya kutoka kwa Imam Sadiq (Amani iwe juu yake):
"إنّ لکلِّ ثَمَرةٍ سمّاً، فإذا أتیتُم بِها فَمَسُّوها بالماءِ – أو اغمِسُوها في الماءِ – یعني اغسِلُوها"
“Kuna sumu juu ya kila tunda, watakapokuletea tunda, basi liweke kwenye maji, au lichovye kwenye maji – Kwa maana: Lioshe” [6].
Kanuni ya jumla ni kula matunda na ngozi yake (kwa maana: Pasina kulimenya tunda na kutoa ngozi yake mfano Apple n.k), hivyo, Kanuni ya jumla kuhusu matunda ni kuyala pamoja na ngozi. Isipokuwa ikiwa kuna tunda ambalo haliwezi kuliwa na ngozi yake au ngozi yake ina madhara (hilo ndilo ambalo litatoka nje ya kanuni hiyo ya jumla).
Kwa mujibu wa riwaya ya Ibn Qadah katika Kitabu cha al-Kafi, Imam Sadiq (Amani iwe juu yake) alichukulia kumenya tunda kuwa ni (ni kitendo cha) karaha (ni makruh) [7] ; Ngozi ya matunda huathiriwa na jua moja kwa moja na ina vitamini mbalimbali na Nyuzinyuzi (Fiber) ambazo ni kwa ajili ya (kurekebisha / kudhibiti harakati ya utumbo, na husaidia kudhibiti au kutibu tatizo la choo kigumu).
Leo hii, kwa sababu mbalimbali, wakulima hutumia sumu na mbolea za kemikali, na wakati mwingine wanazidisha kikomo (kiwango) kinachoruhusiwa; kwa hiyo, ngozi ya matunda inaweza kuambukizwa na sumu hiyo hatari, kwa mantiki hiyo, unapaswa pia kuwa makini (uchukue tahadhari) katika kuteketeza ngozi za matunda hayo, lakini inapotokea ukapata matunda safi na yenye kukuletea afya, na ikawa ngozi zake zinaweza pia kuliwa, basi usipuuze (usighafilike) kabisa kula matunda hayo na ngozi zake.
Kutupa Matunda ambayo sehemu yake (kiasi) yameoza, Matunda yenye ladha chungu na utamu yanapaswa kutupwa mbali [8]. Katika baadhi ya vitabu vya Hadithi, kuna riwaya za kina zaidi ambapo inasemwa ndani yake kwamba Amirul - Muuminina Ali (a.s) alipendekeza kwamba Matikiti Maji (au Matikiti ya Kiajemi _ Persian Melons) ambayo ni machungu au yenye uchachu, au ambayo ni mabovu, yatupiliwe mbali, na yaliwe (yale tu) ambayo ni matamu [9]; ingawa Tikiti Maji ni mojawapo ya matunda yenye majimaji mengi, lakini itakuwa ni ihtimali dhaifu kudhani kwamba kanuni hii ni makhsusi tu kwa matunda kama hayo(yenye majimaji mengi), dhahiri (inavyoonekana) ni kwamba kanuni hii inatumika kwa matunda yote.
Leo hii, inasemekana kwamba ukungu ndani ya matunda huenea zaidi au kidogo katika sehemu zake zote; labda uozo wa matunda unaonyesha kuwa hakuna sumu ya kemikali iliyotumika (katika matunda hayo yakiwa shambani) na kwamba matunda hayo ni salama na yenye afya, lakini ni bora kutumia matunda mengine kutoka kwenye kikapu hicho au mti huo. Kulingana na riwaya hii, ni bora sehemu salama ya tunda lenye ukungu au bovu isitenganishwe na kuliwa (kwa maana kwamba: Usikate sehemu iliyoharibika ya tunda hilo ili ubakishe sehemu salama na uweze kulila). Kuhusu Komamanga; Bwana wa matunda "The lord of fruits", imepokewa kutoka kwa Imam Baqir (Amani iwe juu yake) na Imam Sadiq (Amani iwe juu yake) kwamba:
"مَا عَلَى وَجْهِ الْأَرْضِ ثَمَرَةٌ کَانَ أَحَبَّ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (ص) مِنَ الرُّمَّانِ"
“Hapakuwa na matunda yoyote duniani yaliyokuwa yakipendwa zaidi machoni pa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuliko Komamanga”[10].
Katika Qur'an Tukufu na Hadithi (na Riwaya mbalimbali), majina ya idadi ya matunda ya mbinguni yametajwa, lakini kutokana na mukhtasari wa Hadithi, tunaweza kusema kwamba Komamanga ni Sayyid na Bwana wa matunda yote [11]. Na Riwaya nyingi katika maeneo mahsusi zimezungumzia juu ya majabu na tofauti ya Komamanga, ambapo baadhi ya riwaya hizo zinazungumzia mambo ambayo kamwe hayawezi kupatikana katika matunda mengine ya aina yoyote ile.
Tanbihi (Tiniwayo): [1]. Surah al-Waqiah, Aya ya 20 na 21, [2]. Fiqh al-Mansoob ila al-Imam al-Reza (a.s), Ukurasa wa 347, [3]. Surah Al-An'am, Aya ya 141, [4]. Encyclopedia of Medical Hadiths, Juzuu ya 2, Ukurasa wa 137, 136, Tib al-Nabi', Ukurasa wa 7, Bihar al-An’war, Juzuu ya 62, Ukurasa wa 296, [5]. Tawheed Mufadhal, iliyotafsiriwa na Ali Akbar Mirzai, Ukurasa wa 134, [6]. Al-Kafi, Juzuu ya 6, Ukurasa wa 350, Bihar An’war, Juzuu ya 66, Ukurasa wa 118, Hadithi ya 7, [7]. Al-Kafi, Juzuu ya 6, Ukurasa wa 350, [8]. Dirasat Fi Tib Al-Nabii Al-Mustafa (Utafiti katika Tiba ya Mtume Al-Mustafa), Juzuu ya 4, Ukurasa wa 599, [9]. Bihar al-An’war,Juzuu ya 27, Ukurasa wa 282, Mustadrak al-Wasayli wa Mustambat al-Masayli, Juzuu ya . 16, Ukurasa wa 413 na 414, [10]. Al-Mahasin, Juzuu ya 2, Ukurasa wa 541, namba 833, Al-Kafi, Juzuu ya 6, Ukurasa wa 352, [11]. Al-Mahasin, Juzuu ya. 2, Ukurasa wa 539, Hadithi ya 821.