Katika uchambuzi aliofanya, wa matukio yanayojiri kwenye medani ya vita huko Ghaza, Aluf Benn, mhariri wa gazeti la Haaretz ameandika: "Israel inaingia katika awamu ya pili ya vita dhidi ya Ghaza na itajaribu kukamilisha udhibiti wake wa eneo la kaskazini ya Ghaza hadi Ukanda wa Netzarim. Mhimili wa Netzarim umeanzishwa na jeshi la Israel katikati ya Ukanda wa Ghaza na unaunganisha kaskazini na kusini ya ukanda huo". Benn anaendelea kueleza kwamba, eneo hilo linatayarishwa hatua kwa hatua kwa ajili ya ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi na kuunganishwa na Israel, kwa kutegemea kiwango cha upinzani utakaoonyeshwa kimataifa.Gazeti la Haaretz linatoa madai hayo huku viongozi wa Marekani wakiwa kila mara wanazungumzia kukaribia kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Kwa upande mwingine, Netanyahu na mawaziri wabaguzi wa rangi wa Kizayuni katika serikali yake wanazungumzia kuendeleza vita dhidi ya Ghaza. Ukweli ni kwamba mazungumzo yanayofanyika Cairo na Doha ni ya upotezaji muda tu unaofanywa na Netanyahu na kupunguza mashinikizo ya kimataifa dhidi ya Wazayuni na mshirika wao wa kistratejia, Marekani.
Kutokana na fursa ambayo Marekani na Ulaya zinampatia Netanyahu kwa ajili ya kuwaua Wapalestina ili kufikia malengo yake, kiongozi huyo wa Kizayuni hashughulishwi wala hatiwi wasiwasi na mashinikizo ya kimataifa ya kumtaka asitishe vita dhidi ya Ghaza. Sababu ni kuwa, mashinikizo hayo ni ya kimaonyesho na kiusanii ili kuonyesha kuyajali maandamano yanayofanywa kimataifa kupinga na kulaani mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
Kwa mfano, serikali ya Uingereza imetangaza kuwa imefuta leseni kadhaa za kuiuzia silaha Tel Aviv; lakini unapoisoma kwa undani habari hiyo ndipo inapokudhihirikia wazi kwamba hatua hiyo ya serikali ya London ni ya kimaonyesho na kipropaganda tu.Imeripotiwa kuwa kati ya leseni 350 za kuuuzia silaha utawala bandia wa Israel, ni 50 tu kati ya hizo zimefutwa. Kwa hatua yake hiyo, Waziri Mkuu wa Uingereza na kiongozi wa chama tawala cha Leba Keir Starmer anataka kuonyesha kwamba sera yake kuhusiana na utawala wa Kizayuni ni tofauti na ya chama cha Wahafidhina, ilhali ukweli ni kuwa hakuna tofauti yoyote kati ya chama cha Leba na kile cha Wahafidhina katika sera za Uingereza kuhusiana na Mashariki ya Kati. Uungaji mkono kamili na wa kila hali kwa utawala bandia wa Israel ndicho kitovu na nukta kuu ya sera ya Uingereza katika Mashariki ya Kati.
Marekani na nchi nyingine za Ulaya haziko tayari hata kwa sura ya kimaonyesho na kipropaganda kuweka kikomo au kusimamisha usafirishaji wa silaha zinazoupatia utawala wa Kizayuni na kuwawekea Wazayuni vikwazo. Kile ambacho Marekani na serikali za Ulaya zimekuwa zikijinasibu kwacho, yaani kujali na kutetea haki za binadamu zimekipoteza kwa kuwasaidia na kuwaunga mkono Wazayuni katika mauaji ya kimbari wanayofanya dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.Sasa hivi kuna habari mbili zinazosikika duniani kutoka Ulaya na Marekani kuhusu msimamo unaoonyeshwa kwa jinai zinazofanywa na Wazayuni huko Ghaza. Habari ya kwanza ni ya misimamo legevu ya kutochukuua hatua yoyote serikali za Ulaya kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Wapalestina. Na habari ya pili ni ya matukio yanayojiri mabarabarani na kwenye vyuo vikuu vya Ulaya na Marekani.Kwa hakika hakuna siku wala wiki inayopita pa sina kushuhudiwa na kuripotiwa mikusanyiko na maandamano, hasa yanayofanywa na kizazi cha vijana wa Marekani na wa nchi za Ulaya, ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani jinai za Wazayuni. Kwa muqawama ulioonyeshwa na Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, Wazayuni hawataweza kutimiza ndoto zao za kuinyakua na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya Palestina.
Tumalizie kwa kusema, dhati ya ubaguzi wa rangi, uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu ya utawala bandia wa Israel sasa imefichuka na kudhihirika zaidi mbele ya macho ya walimwengu.../