Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

13 Septemba 2024

20:40:56
1484898

Kiongozi wa Hamas amuandikia barua Kiongozi wa Hizbullah, asisitiza kuishinda Israel

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Yahya Sinwar amemuandikia barua kiongozi wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyed Hassan Nasrallah, akiahidi kwamba harakati hiyo ya muqawama au mapambano ya Kiislamu "itasalia imara" katika njia ya kuushinda utawala haramu wa Israel.

Barua ya Sinwar siku ya Ijumaa imeandikwa kujibu ujumbe wa rambirambi wa Sayyid Hassan Nasrallah kufuatia mauaji ya kiongozi wa zamani wa Hamas Ismail Haniyah mjini Tehran.

Katika barua hiyo, Sinwar akiashiria kufa shahidi Ismail Haniyah na mlinzi wake katika shambulizi hilo la kigaidi lililotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel amesema: "Sisi katika Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina tumepokea kwa shukrani na fahari ujumbe wako mzuri wa kuwaomboleza mashahidi wetu wawili na masahibu wako katika jihadi na muqawama."  

Haniyah aliuawa shahidi mwezi Julai akiwa na mlinzi wake katika makazi yake kaskazini mwa Tehran baada ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.

Sinwar alimsifu Haniyah kama "nembo ya taifa la Palestina", akisema damu yake na damu ya Wapalestina wengine itaongeza nguvu na uwezo wao "katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Kinazi".

Aidha kiongozi huyo wa Hamas amesema watu wa Palestina wana umoja na wamechagua  jihadi na muqawama katika kukabiliana na mradi wa Kizayuni na kuongeza kwamba, Wapalestina watalinda matakatifu yao ambayo ni mji wa al-Quds na Msikiti wa al-Aqsa.

342/