Katika taarifa yake Ijumaa usiku, Hizbullah ilimmiminia sifa tele kamanda wake huyo aliyeuawa shahidi. Taarifa hiyo imesema: "Kiongozi mkubwa wa jihadi, Hajj Ibrahim Aqeel [Hajj Abdul Qader], amejiunga na safu ya ndugu zake waliouawa shahidi, viongozi bingwa waliomtangulia."
Hali kadhalika taarifa hiyo imesema: "Maisha yake yalikuwa ya kujitolea bila kuyumba, yalikuwa maisha ya jihadi, ustahimilivu, na kujitolea bila kubadilika hata wakati wa matatizo."
Aidha Hizbullah imesema: “Al-Quds (Jerusalem) ilikuwa daima katika moyo na akili yake, mchana na usiku. Ilikuwa ni shauku yake kubwa zaidi na alikuwa na matarajio makubwa kuwa siku moja ataweza kuswali katika Msikiti Mtakatifu wa Al-Aqsa. Hizbullah imeapa kuendeleza lengo lake la kuikomboa Quds Tukufu hadi ushindi wa mwisho, Mwenyezi Mungu akipenda."
Hajj Aqil alijiunga na Hezbollah katika miaka ya 1980 na alihusika na operesheni za kundi hilo la muqawama dhidi ya Israel.
Mapema siku ya Ijumaa, utawala wa Israel ulitekeleza hujuma katika mji wa Beirut na kuua takriban watu 14 na kujeruhi wengine 66.
Kulingana na Shirika rasmi la Habari la Kitaifa la Lebanon (NNA), watoto watano ni miongoni mwa waliouawa katika hujuma hiyo ya kigaidi ya Israel.
Kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon imesema ndege isiyo na rubani ilivurumishha makombora kadhaa katika kitongoji cha Dahiyeh chenye wakazi wengi mjini Beirut. Nalo Shirika rasmi la Habari la Kitaifa la Lebanon limesema ndege ya kivita aina ya F35 ilitumika katika hujuma hiyo.
342/