Main Title

source : Abna
Alhamisi

10 Oktoba 2024

05:31:15
1493266

Iraq yalaani njama ya Israel ya kumuua Ayatullah Sistani

Serikali ya Iraq imelaani vikali njama ya utawala haramu wa Israel ya kutaka kumuua kiongozi mkuu wa Kiislamu nchini humo Ayatullah Sayyid Ali Sistani.

Taarifa iliyotolewa leo na serikali ya Iraq, imezitaka taasisi zote za Umoja wa Mataifa na kimataifa kulaani na kukemea jambo lolote linalogusa hisia za Waislamu wote duniani.
Kauli hiyo imekuja baada ya Kanali ya 14 ya Televisheni ya utawala haramu wa Israel kuonyesha picha ya kiongozi wa juu zaidi ya Kiislamu nchini Iraq, Ayatullah Sistani, kama mmoja wa walengwa wa mipango ya mauaji ya kigaidi ya Israel.
Picha ya Ali Sistani ilionekana pamoja na picha za kiongozi wa Harakati ya Ansarullah, Abdul Malik Al-Houthi, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) Yahya Al-Sinwar, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ismail Qaani, na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Televisheni hiyo ya Israel - ambayo iko karibu na Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu - ilichapisha taswira hizo jana, Jumanne, zikiambatana na neno "shabaha" kwenye kichwa cha kila mmojawao.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, Israel haijawahi kuzungumza hapo awali kuhusu suala la kumuua kigaidi Ayatullah Sistani, ingawa baadhi ya maafisa wake walitaja majina ya wengine wote ambao picha zao zimeonyeshwa na idhaa hiyo kama "shabaha" kwenye orodha ya mauaji ya Israel.
Ayatullah Ali Sistani - aliyezaliwa mwaka wa 1930 - ni marja' na kiongozi wa ngazi ya juu kabisa wa kidini kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq na maeneo mengine ya dunia na anaishi katika mji mtakatifu wa Najaf katikati mwa Iraq. 

 IQNA