Tukio la kusikitisha la Karbalaa
Tukio lilomtokea Imam Husein:
Jina lake kamili ni Husein bin Ali bin Abitwalib, baba yake ni ndugu wa mtume na swahaba wake wakaribu zaidi kuliko wengine, baba wa Husein, ambaye ni Ali bin Abitwalib, alisifika kwa elimu ya juu na ushujaa usio na kifani, Mama wa Husein ni Fatma bint wa mtume Muhammad s.a.w , bibi yake ni Bi Khadija mke wa mtume Muhammad s.a.w.
Husein alizaliwa siku ya Alhamisi, tarehe tatu mwezi Sha’aban mwaka wa nne Hijiria(3rd Sha'aban 4 AH) sawa na (8 Januari mwaka 626), Husein ni mtoto wa pili wa Sayyida Ali na Bi Fatma, ambapo alitanguliwa na kaka yake aitwaye Hasan.
Tangu akiwa mdogo yeye na kaka yake walitumia muda mwingi sana wakiwa karibu na babu yao, ambaye ni mtume Muhammad s.a.w. Husein tangu akiwa mdogo alionekana ni shujaa na mwenye hekima ya hali ya juu.
Imamu Husein aliishi na mtume kwa muda wa miaka minane, ambapo mtume Muhammad s.a.w alifariki dunia, katika kipindi hichi chote alipata mafunzo na malezi ya kiislamu kutoka kwa mjumbe na mtume wa uislamu Muhammad s.a.w. baada ya mtume Muhammad s.a.w Husein alikuwa miongoni mwa wasaidizi wa katibu wa baba yake na alipofikisha miaka thelathini na saba, baba yake alifariki,baada ya baba yake kufariki, Husein alikuwa msaada mkubwa kwa kaka yake, Imam Hasan, ambapo alikuwa bega kwa bega na kaka yake na kumsaidia katika masuala ya uongozi wake wa dini tukufu ya uislamu. Baada ya kifo kaka yake, Husein alishika madaraka ya kaka yake, kama kiongozi wa dini ya tukufu ya mtume Muhammad s,a,w na aliongoza kwa muda wa muongo mmoja, aliendelea na uongozi wake wa dini mpaka siku ya kumi ya mwezi wa Muharram ambayoni maalufu kama siku ya Ashuraa, ambapo aliuawa kikatili na wapinzani wake ambao walitaka madaraka ya kuuongoza uislamu, hivyo walimuua mjukuu wa mtume Muhammad s.a.w ili wachukue nafasi ya uongozi wa umma wa kiislamu baada yake. Imam husein a.s aliuawa akiwa na umri wa miaka hamsini na saba.
Husein bin Ali anahesabika kuwa ni miongoni mwa watu muhimu katika uislamu na anaheshimiwa na madhehebu yote ya kiislamu ila anaheshimiwa na kupewa zaidi cheo chake na waislamu wa dhehebu la shia, ambao ndio wafuasi wake.
Husein bin Ali bin Abi twalib ni mtu wa pekee aliyeuawa kinyama katika historia ya uislamu, na ni katika watu watukufu waliouawa kwa ajili ya kutetea dini ya mtume Muhammad s.a.w.
Kwa Muhtasari ni kwamba: Baada ya kufariki mtume Muhammad s.a.w, kulitokea tofauti kati ya waislamu kuhusu nani atakayeshika madaraka ya kuuongoza umma wa kiislamu baada ya mtume Muhammad s.a.w. katika hali hii waislamu waligawanyika makundi makuu mawili.
Wako waliojikusanya na kumchagua kiongozi ambaye ni Abu bakar bin kuhafah na wengine walisukuti wakiendelea na maandalizi ya mazishi ya mtume Muhammad s.a.w. watu hawa walisukuti kwa kuwa wanaamini kuwa mtume kabla ya kufariki aliacha usia kuwa Ali bin Abi twalib ndiye atakaye kuwa kiongozi baada yake.
Kundi la kwanza ndio wale wanaoitwa Ahlusunna hivi sasa, na kundi la pili ndio wanaitwa mashia, baada ya kufariki Abubakari kwa mujibu wa siasa za kundi la Sunni, madaraka ya kuongoza uislamu yalichukuliwa na Omar bin Khatwab, kisha Uthman bin Affan kisha Ali bin Abitwalib kisha Muawiyah kisha Yazid bin Muawiyyah na wengineo.
Kundi la Shia halikukubaliana kabisa na utawala huu, uliokuwa ukiendelea, hivyo walipewa jina la kisiasa la “Rafidhwa” likiwa linamaana ya wapinzani. Jina hili si laiki wala si chaguo la mashia bali Ahlusunna waliwaita mashia kwa jina hilo kutokana na upinzani wao dhidi ya makhalifa walioko madarakani, Shia waliendeleza msimamo wao wa kumfuata Ali bin Abi twalib kama kiongozi wao wa kwanza na akafuatia mtoto wa Ali ambaye ni Hassan na kisha akafuatia Husein.
Kifupi, mashia wanaamini kwamba uongozi wa uislamu baada ya mtume, hauji kwa njia ya demokrasia kwamba watu wakae na kumchagua khalifa, bali mtume ndiye mwenye haki ya kuanisha na kuteua atakayekuwa khalifa baada yake, na kwamba mtume aliondoka ameshachagua viongozi watakaongoza umma wa kiislamu, ambapo viongozi hawa wanatoka katika kizazi chake mtume Muhammad s.a.w (Ahlul bayt).
Ilivyo ada kwa waarabu mtu anapotaka uongozi ni lazima akubaliwe na wakuu wa makabila au watu wenye cheo na shahasia ya juu, kwani hiyo itakuwa ni sababu ya yeye kukubaliwa na kila mfuasi wa wakuu hao, hivyo viongozi hao huwa wanafuata wakuu hao na kuwaomba watoe kiapo chao cha utii kwa viongozi wapya.
Baada ya kufariki Muawiyah bin Abi Sufyaan, uongozi wa Ahlusunna alishikiriwa na mwana wa Muawiyah ambaye ni Yazid, Yazid alipita kwa viongozi wa makabila na wakuu wa kijamii kuchukua kiapo cha utii, kila aliyekataa kumuunga mkono alimuua.
Yazid bin Muawiya anatuma majeshi yake kwa Husein bin Ali yakachukue kiapo cha utii, na anatoa agizo kwamba ikiwa atakataa au kupinga basi auawe. Habari inamfikia Husein bin Ali akiwa Makka ambapo watu wa Iraq wanamtumia barua nyingi kumwita aende Iraq, Husein bin Ali anaona si laiki wa si sahihi kama yeye atauawa ndani ya mji mtukufu wa Makka ambao kumeharamishwa mauaji katika sehemu hiyo, na anajua fika kabisa kuwa hatima yake itakuwa ni kuuawa, popote atakapo kuwa hata kama atakuwa katika Kaaba tukufu.
Hapo ndipo Husein bin ali anakata shauri la kusafiri kuelekea Iraq akiwa na familia yake, akiongozana sanjari na wafuasi wake.
Akiwa katika safari yake, alipofika katika sehemu Moja iitwayo Karbal, majeshi ya yazid yalimzuia Husein kuendelea na msafara na kumtaka atoe kiapo cha utii, Husein ambaye pia ni mjukuu wa mtume Muhammada s.a.w alipinga katakata kutoa kiapo cha utii kwa Yazid, kwani kufanya hivyo ni kuruhusu ufisadi na uovu utawale uislamu.
Hivyo walipomwambia atoe kiapo cha utii kwa Yazid aliwajibu kwa kusema”Yeyote aliyoko kama mimi, hawezi kutoa kiapo cha utii, kwa mtu yeyote aliyemfano wa Yazid ”.
Wanajeshi hao walimwambia basi hatuna budi kuua. Husein aliwajibu”Kufa kwa heshima ni bora kuliko kuishi kidhalili”
Aliendelea kuwambia kuwa “mimi siko hapa kwa ushari, au kutaka ugomvi ila niko hapa kwa ajili ya kurejesha heshima ya dini tukufu ya babu yangu mtume Muhammad s.a.w, niko hapa kuamrisha mema na kukataza uovu, niko hapa kusahihisha itikadi na imani za waislamu”.
Jehi la Yazid lilimua Husein , watoto wake na wafuasi wake, waliua hata watoto wadogo na kisha waliwateka wanawake na watoto waliosalia katika familia ya Husein bin Ali.
Walikata kichwa cha Husein mjukuu wa mtume Muhamad s.a.w na kukining’iniza juu ya mkuki na kukipeleka kwa Yazid bin Muawiya Sham (Syria).
Tukio hili lilitokea siku kama ya leo siku ya kumi mwenzi wa Muharam mwaka wa 61 hijiria (10/1/61) sawa na 10 October mwaka 680.
Siku ya leo ni siku ya huzuni kwa waislamu wa madhehebu ya Shia, na wapenda haki duniani kote.
Mamilion ya waislamu na wapenda haki kote duniani wanaadhimisha siku hii, wengine wanachangia damu katika mahospitali katika maadhimisho haya.
Amani iwe na Husein, pamoja na kizazi chake na maswahaba wake.