Main Title

source : Pars Today
Jumanne

21 Mei 2019

08:28:25
943111

Kutangazwa msimamo wa Russia wakati wa kukaribia uzinduzi tarajiwa wa mpango wa "Muamala wa Karne"

Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuzingatia himaya na uungaji mkono wa pande zote wa Rais Donald Trump wa Marekani umekuwa ukitekeleza mashinikizo ambayo hayajawahi kushudiwa dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina na kufanya mambo kinyume kabisa na sheria za kimataifa.

(ABNA24.com) Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuzingatia himaya na uungaji mkono wa pande zote wa Rais Donald Trump wa Marekani umekuwa ukitekeleza mashinikizo ambayo hayajawahi kushudiwa dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina na kufanya mambo kinyume kabisa na sheria za kimataifa.

Mfano wa wazi ni mpango wa serikali ya Marekani unaojulikana kwa jina la "Muamala wa Karne", ambao kimsingi umeandaliwa maalumu kabisa kwa ajili ya kuhudumia maslahi ya utawala ghasibu wa Israel. Jambo hilo limekabiliwa na radiamali kutoka kwa Russia moja ya madola makubwa duniani na ambalo lina uhusiano mkubwa na Wapalestina. Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Jumamosi ya juzi tarehe 18 Mei alipokea barua ya Rais Vladimir Putin wa Russia inayohusiana na himaya na uungaji mkono wa Moscow wa uhalali wa Palestina kimataifa.

Haidar Aghanin, balozi wa Russia mjini Ramallah ndiye aliyemkabidhi Mahmoud Abbas barua ya Rais Putin. Katika barua yake hiyo kwa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Rais Putin amesema: Russia ina wasiwasi na juhudi zozote zile zenye lengo la kukanyaga sheria za Umoja wa Mataifa na kanuni za kimataifa. Rais Putin ameashiria matukio ya Quds inayokaliwa kwa mabavu na mpango wa "Muamala wa Karne" na kusisitiza kwamba: Russia inaunga mkono uhalali wa kimataifa wa Palestina.

Rais wa Russia anaashiria mpango wa "Muamala wa Karne" katika hali ambayo, serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imekuwa ikiufuatilia mpango huo kwa nguvu zake zote na filihali imo mbioni kuutangaza na kuutekeleza kivitendo. 

Kwa mujibu wa mpango wa Marekani wa 'Mumala wa Karne', mji wa Quds utakabidhiwa kwa Israel, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki ya kurejea makwao, utawala haramu wa Israel utasimamia usalama wa sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vivuko vya mpakani huku maeneo pekee ya Kiarabu ya Quds Mashariki yakiunganishwa na nchi ya Palestina. Aidha kwa mujibu wa mpango huo, nchi ya Palestina haitakuwa na jeshi.

Donald Trump amemteua Jared Kushner ambaye ni mkwewe kuwa dalali wa kuupigia upatu muamala huo uliojaa njama dhidi ya Wapalestina. Kwa mtazamo wa Moscow ni kuwa, mpango wa "Muamala wa Karne" unakinzana bayana na maazimio ya Umoja wa Mataifa pamoja na sheria za kimataifa. Hata Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo yenyewe hadi sasa imechukua hatua nyingi za kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel inaouna mpango huo kuwa, si wenye kukubalika hata kidogo.

Akihutubia miezi kadhaa iliyopita kwa mnasaba wa mwaka wa 54 wa kuasisiwa Harakati ya Fat'h, Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alisema kuwa, katu hatutamruhusu Donald Trump aiuze Quds kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Rais Donald Trump ametoa huduma kubwa kwa utawala haramu wa Israel mambo ambayo viongozi wa ngazi za juu wa Israel hususan Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hakuwa hata akiyaota usingizini.

Serikali ya Trump ni muungaji mkono mkuu wa utawala dhalimu wa Israel kupitia misaada yake mbalimbali ya kifedha na kisilaha. Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa mwaka Marekani huipatia Israel misaada yenye thamani ya dola bilioni tatu na milioni 800 katika uwanja huo.

Katika upande mwingine, Machi 25 mwaka huu, Rais wa Marekani alitangaza kutambua rasmi udhibiti na umiliki wa utawala vamizi wa Israel kwa miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.

Aidha mwezi Mei mwaka jana, Marekani ilichukua hatua ya kichochezi na ambayo inakinzana waziwazi na maazimio yote ya kimataifa ya kuhamishia ubalozi wake katika mji wa Beitul-Muqaddas kutoka Tel Aviv.

Miongoni mwa uungaji mkono mwingine na himaya za Marekani kwa utawala haramu wa Israel ambazo tunaweza kuziashiria ni hatua ya Washington ya kulikatia misaada Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), kumtimua balozi wa Palestina kutoka Washington na kufunga akaunti zake.

Filihali Trump anakusudia kutambua rasmi kuunganishwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na ardhi zaPalestina zinazokaliwa kwa mabavu na hatua itakayofuata autangaze mpango wa "Muamala wa Karne" na kwa muktadha huo akamishe utoaaji wake wa huduma kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Pamoja na hayo upinzani mkubwa wa Palestina, kushuhudiwa upinzani huo pia kieneo na kimataifa dhidi ya hatua hizo za Donald Trump ukiwemo mpango wa "Muamala wa Karne" ni mambo ambayo yametilia shaka kama kweli mpango huo utatekelezwa kivitendo.



/129