Main Title

source : Pars Today
Jumapili

9 Juni 2019

07:41:17
948518

Uchochezi wa Saudi Arabia na Imarati katika mgogoro wa Sudan

Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ulishadidi Juni 3 baada ya wanajeshi kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wamekusanyija nje ya makao makuu ya jeshi ambapo raia zaidi ya 100 waliuawa katika vurumai hiyo.

(ABNA24.com)  Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ulishadidi Juni 3 baada ya wanajeshi kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wamekusanyija nje ya makao makuu ya jeshi ambapo raia zaidi ya 100 waliuawa katika vurumai hiyo.

Matukio ya nchini Sudan katika muongo mmoja uliopita yanaonyesha kuwa ajinabi wamekuwa wakiingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na hapa tunaweza kutaja nafasi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuivunja nchi hiyo katika vipande viwili vya Sudan na Sudan Kusini. Katika mgogoro wa hivi sasa wa Sudan pia, madola ajinabi yanaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ambapo Saudi Arabia na Imarati zimetajwa kuwa na nafasi kubwa katika kuliunga mkono jeshi ambalo linawakandamiza wananchi kwa lengo la kunyakua madaraka kikamilifu. Kuna ushahidi unaoashiria namna madola hayo mawili ya Kiarabu yanavyoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Awali kabisa: Katika kipindi cha miaka 9 iliyopita, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE- (Imarati) zimethibitisha kuwa zimekuwa zikichua hatua za kukandamiza na kuzuia mwamako wa wananchi wanaotaka demokrasia katika nchi za Kiarabu. Saudi Arabia imetajwa kuwa kinara wa wapinzani wa mapinduzi ya wananchi katika nchi za Kiarabu. Tokea Disemba mwaka 2018, wananchi wa Sudan walianzisha maandamano yao dhidi ya utawala wa kiimla wa Rais Omar al Bashir. Hatimaye mnamo Aprili 11 mwaka huu, walifanikiwa kumlazimisha al Bashir kuondoka madarakani baada ya utawala wake wa miongo mitatu. Baada ya al Bashir kutimuliwa, Baraza la Mpito la Kijeshi lilichukua mamlaka ya uongozi na kuna ushahidi wa wazi kuwa, baraza hilo linaungwa mkono na Saudia pamoja na Imarati. Tawala hizo mbili za Kiarabu zilikuwa nchi za kwanza kulitambua rasmi Baraza la Mpito la Kijeshi Sudan. 

Gazeti la al Quds al Arabi limeandika hivi kuhusu kadhia hiyo: "Siku tatu tu baada ya kupinduliwa al Bashir, Mfalme wa Saudi Arabia alitoa amri ya kutuma shehena kubwa ya dawa na chakula nchini Sudan."

Nukta ya pili ni kuwa: Katika siku za tarehe 30 na 31 Mei mwaka huu, Saudi Arabia iliitisha vikao vya wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC katika mji wa Makka, ambapo kiongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan Abdul Fattah al Burhan naye pia alialikwa. Katika kikao hicho cha Makka, al Burhan alikutana na Mrithi wa Ufalme wa Saudia Mohammad bin Salman. Lengo la Saudia kumualika al Burhan lilikuwa ni kutuma ujumbe kuwa, Saudia inamtambua kama mtawala rasmi wa Sudan. Hii ni katika hali ambayo wananchi wa Sudan wamekuwa wakiandamana wakitaka al Burhan na baraza lake la mpito la kijeshi waondoke madarakani na nafasi yao ichukuliwe na baraza la mpito la kiraia. Siku mbili tu baada ya al Burhan kurejea kutoka Saudia, wanajeshi wa Sudan ambao katika miezi kadhaa ya maandamano wamekuwa wakijizuia kuwashambulia raia, mara hii walipokea amri ya kufyatua risasi ambapo waliwaua zaidi ya raia 100 kwa mpigo. Duru za Sudan zinasema mauaji hayo ya Jumatatu iliyopita katika mji wa Khartoum yalitekelezwa kwa uungaji mkono na himaya kamili ya Saudia na Imarati.

Dkt. Taj Al Ser Othman, msomi na mwanafikra wa Sudan katika ujumbe wake kupitia Twitter ameashiria kushiriki mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan katika kikao cha Makka na kuandika: "Waandamanaji wa  Sudan waliokuwa katika Saumu wameuawa kwa fedha za mafuta kutoka Saudi Arabia.

Nukta ya tatu ni kuwa: Baadhi ya duru za habari siku ya Ijumaa zilidokeza kuwa, Khalid bin Salman ambaye ni kaka yake mdogo Mohammad bin Salman, Anwar  Gargash, Waziri Mshauri wa Mambo ya Kigeni Imarati na Mohammed Dahlan, mshauri wa Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed al Nahyan, walifanya safari ya siri hivi karibuni nchini Sudan. Taarifa zinasema walipowasili mjini Khartoum walilakiwa  na Mohammad Hamdan Dagalo kamanda wa vikosi maalumu vya Sudan. Safari hiyo ya siri imefanyika kwa ajili ya kujaribu kuliondoa jeshi la Sudan hasa Abdul Fatah al Burhan katika kinamasi na mgogoro mkubwa wa sasa ambao umeshadidi baada ya kuuawa na kujeruhiwa mamia ya waandamanaji.

Nukta ya mwisho ni kuwa, weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa, Saudia na Imarati zinataka kutumia ile mbinu iliyotumika kumuingiza Jenerali  Abdul Fatah el Sisi madarakni nchini Misri kwa ajili ya kumuwezesha Luteni Jenerali Abdul Fatah al Burhan naye achukue madaraka nchini Sudan na hivyo kuyafanya mapinduzi ya wananchi yaambulie patupu.

Sami Kamal al Din, mwanahabari na mchambuzi wa Misri anasema mauaji ya Jumatatu iliyopita mjini Khartoum ni sawa na mauaji ya Agosti 2013 katika Medani ya Rabaa mjini Cairo.




/129