Main Title

source : Pars Today
Jumatatu

15 Julai 2019

05:56:41
961151

Sisitizo la Erdoğan la kutosahaulika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2016 nchini Uturuki

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesisitizia udharura wa kutosahaulika jaribio la mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai 2016 dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

(ABNA24.com) Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter Erdoğan ameandika: "Kukumbukwa mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2016 nchini Uturuki, ni tukio lisilosahaulika. Na sisi hatutoruhu mapinduzi hayo yasahaulike." Matamshi ya rais wa Uturuki juu ya kutosahaulika mapinduzi hayo ya kijeshi ya Julai 2016, ni yenye umuhimu kwa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi nchini humo. Ukweli ni kwamba jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi ambalo lilitokea tarehe 15 Julai 2016 dhidi ya serikali ya Rais Erdoğan liliandaa uwanja wa kufikiwa matakwa yote ya ndani yaliyokuwa yakifuatiliwa na rais huyo, hasa katika kipindi cha tukio hilo. Kwa hakika mapinduzi hayo yaliyofeli, yaliharakisha malengo ya muda mrefu ya Erdoğan nchini Uturuki. Katika hali ambayo serikali ya Ankara inasisitizia ulazima wa kufanyika kumbukumbu za mwaka wa tatu wa tukio hilo, wapinzani wa Rais Erdoğan wakosoa mipango ya kufanyika kumbukumbu hizo. Kwa mfano, Bülent Tezcan, Naibu Katibu Mkuu wa chama cha CHP, amemtuhumu Erdoğan kwa kupindisha tukio la mapinduzi hayo ya kijeshi yaliyofeli ya mwaka 2016 dhidi ya serikali ya Ankara, kwa maslahi yake binafsi. Kuhusiana na suala hilo, Tezcan anasema: "Serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan inatumia kumbukumbu za mapinduzi ya tarehe 15 Julai 2016 kwa lengo la kuandika historia bandia."

Aidha mwanasiasa huyo wa Uturuki amedai kwamba, rais wa nchi hiyo amezuia kufanyika uchunguzi kuhusiana na tukio hilo la mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli. Inafaa kuashiria kuwa, siku tano baada ya kujiri jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi mwala 2016, yaani tarehe 20 Julai mwaka huo, bunge la Uturuki lilipitisha muswada wa sheria ya hali ya hatari, ambayo ilitakiwa kutekelezwa tu na serikali ta Erdogan bila ya uingiliaji wa mihimili mingine ya serikali. Kiasi kwamba serikali hiyo ilitumia vibaya sheria hiyo kuwakandamiza wapinzani wa serikali kwa visingizio tofauti, kuwatia mbaroni na kuwafunga jela. Wakati huo huo, siasa za ndani na nje za Uturuki zote ziliwekwa moja kwa moja mikononi mwa Rais Erdoğan ambapo binafsi aliweza kuchukua maamuzi mbalimbali muhimu katika uwanja huo. Kuendelea kurefushwa sheria ya hali ya hatari kunakofanywa na chama tawala cha Uadilifu na Ustawi katika bunge la nchi hiyo, kumeubua upinzani mkali dhidi ya serikali ya Ankara. Katika uwanja huo, wapinzani wa serikali ya Erdogan wanasisitiza nukta hii kwamba, chama tawala kinakusudia kurefusha hali ya hatari hadi mwezi Novemba mwaka huu, yaani hadi wakati ambao raia wa nchi hiyo wataelekea kwenye masunduku ya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua moja kwa moja rais wa nchi kinyume na huko nyuma ambapo rais amekuwa akichaguliwa na chama kilicho na wingi wa viti bungeni.

Kuhusiana na suala hilo Sennan Serhan, mtaalamu wa masuala ya sheria na mmoja wa wanaharakati wa kisiasa nchini humo anasema: "Tangazo muhimu la hali ya hatari nchini Uturuki, ni kinyume cha sheria. Hali ya hatari inatakiwa kutangazwa tu wakati kunapotokea machafuko yasiyoweza kudhibitiwa. Hii ni katika hali ambayo mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 15 Julai 2016 yalitokea katika miji ya Ankara na Istanbul tu tena katika kipindi cha chini ya masaa sita na yakawa yamesambaratishwa." Tunaweza kusema kuwa, kwa kuzingatia faida iliyoipata serikali ya Rais Erdoğan kutokana na mapinduzi hayo yaliyofeli ya mwaka 2016, kufanyika marasimu ya kumbukumbu za tukio hilo, ni jambo la kawaida. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, mapinduzi hayo yamewaandalia viongozi wa Ankara mazingira yanayofaa kwa lengo la kuwafuatilia kwa karibu wapinzani wao.



/129