(ABNA24.com) Zoezi la kuanza kuikabidhi Uturuki mfumo wa kujilinda kwa makombora wa S-400 lilianza siku ya Ijumaa ya tarehe12 Julai na hadi hivi sasa shehena 15 za mfumo huo zimeshafikishwa katika kituo cha anga cha Mürted huko Akıncı, katika viunga vya Ankara. Hivyo viongozi wa Marekani wamepata yakini kwamba Uturuki haina nia kabisa ya kuvunja mkataba wake na Russia wa kununua mfumo huo wa S-400 wa kujlinda na mashambulizi ya anga na makombora. Kama ilivyotarajiwa, Marekani nayo imeamua kujibu hatua kwa hatua uamuzi huo wa Uturuki.
Hivi sasa Marekani imeamua kutekeleza kivitendo uvumi ulioenea huko nyuma kwamba ina nia ya kuvunja mkataba wake na Uturuki wa kushirikiana na Ankara katika utengenezaji wa mradi wa ndege za kivita za kizazi cha tano za F-35. Ikulu ya Marekani, White House, imetangaza rasmi kuwa imevunja mkataba wake huo na Uturuki. Taarifa ya White House imesema: Inasikitisha kuona kuwa uamuzi wa Uturuki wa kununua mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya anga wa S-400 kutoka kwa Russia unaendelea hivyo unalifanya suala la kushiriki Uturuki katika mradi wa ndege za F-35 usiwezekane tena. Mradi wa ndege za F-35 hauwezi kuwa mahala palipo na jukwaa la kukusanya taarifa la Russia. Ikulu ya Marekani imeongeza kuwa, hatua ya Uturuki ya kununua mfumo wa S-400 kutoka kwa Russia utaathiri pia uhusiano wake na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi, NATO.
Katika tukio jingine, Washington imewataka marubani wa Uturuki wawe wameshaondoka nchini Marekani ifikapo tarehe 31 mwezi huu wa Julai. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani amesema mbele ya waandishi wa habari kwamba, Washington imeanza rasmi mchakato wa kuitoa Uturuki katika mradi wa kuunda ndege za kivita za F-35. Hatua ya Uturuki ya kununua mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 haioani na suala la kushirikiana kwetu na nchi hiyo katika NATO.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ijapokuwa Marekani imeamua kutekeleza kivitendo vitisho vyake dhidi ya Uturuki, lakini wakati huo huo Washington imeshindwa kuficha hamu yake ya kuhakikisha kuwa Ankara haitoki mikononi mwake. Ndio maana katika taarifa yake Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imetangaza kuwa hatua zote zilizochukuliwa dhidi ya Uturuki zinaweza kuondolewa kwa sharti kwamba Ankara ivunje mkataba wake na Russia wa kununua mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400. Imetangazwa pia kuwa, Washington itafanya juhudi zake zote kuhakikisha kuwa Uturuki inapatiwa mfumo madhubuti wa ulinzi wa anga wenye viwango vya NATO na hatimaye kuirejesha nchi hiyo katika mradi wa kutengeneza ndege za kivita za F-35.
Suala hilo hata hivyo halikupokewa vizuri na Uturuki. Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Mevlüt Çavuşoğlu ameitaka Marekani ibadilishe uamuzi wake wa kuitoa Ankara katika mradi wa kutengeneza ndege za kivita za F-35. Amesema: Uamuzi wa Washington wa kuitoa Uturuki katika mradi wa kutenengeza ndege za kivita za F-35 si uadilifu na ni kinyume cha sheria. Uamuzi huo wa Marekani utaharibu uhusiano wetu wa kiistratijia na Washington.
Hata hivyo dalili zote zinaonesha kuwa Marekani haitobadilisha uamuzi wake wa kuichukulia hatua Uturuki baada ya Ankara kununua mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 kutoka Russia. Si hayo tu, lakini pia kuna uwezekano Washington ikaichukulia hatua kubwa zaidi Ankara hasa kwa kuzingatia kuwa Baraza la Congress la Marekani limeitaka nchi hiyo kuiwekea vikwazo Uturuki kwa mujibu wa sheria ya CAATSA.
/129