Main Title

source : Pars Today
Jumamosi

20 Julai 2019

07:58:24
962824

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain akiri kuanzishwa uhusiano wa nchi yake na Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain amekariri tena madai yake kwamba kuanzishwa uhusiano wa nchi hiyo na utawala haramu wa Israel ndio 'msingi wa amani halisi' katika eneo la Asia Magharibi.

(ABNA24.com) Hamu ya Bahrain kuanzisha uhusiano rasmi na wa wazi na utawala ghasibu wa Israel si siri tena bali serikali ya Manama inataka uhusiano huo uanzishwe haraka iwezekanavyo. Hali hiyo inabainika wazi katika matamshi na misimamo ambayo imekuwa ikichukuliwa na utawala huo katika miezi ya hivi karibuni kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Khalid bin Ahmad bin Muhammad Aal Khalifa.

Bahrain ilikuwa mwenyeji wa kikao cha uchumi kilichoandaliwa mjini Manama tarehe 25 na 26 za mwezi Juni kwa lengo la kutekeleza kivitendo mpango wa Marekani na utawala wa Kizayuni, wa Muamala wa Karne. Ni wazi kuwa mpango huo unaodhamini maslahi haramu ya Israel katika Asia Magharibi unapingana wazi na malengo matukufu ya taifa la Palestina. Ni kutokana na ukweli huo ndio maandamano makubwa ya kupinga mpango huo na utawala wa Aal Khalifa yakafanyika ndani na nje ya Bahrain. Wakati wa kufanyika kikao hicho, Khalid bin Ahmad bin Muhammad Aal Khalifa alitangaza wazi katika mahojiano na vyombo vya habari vya utawala wa kibaguzi wa Israel kwamba Bahrain ilikuwa imechukua uamuzi wa kuanzisha uhusiano rasmi na utawala huo. Akizungumza jana pia katika Chuo cha Baraza la Atlantic, ambapo  Bryan Hook, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran alihudhuria, Ahmad bin Muhammad Aal Khalifa alidai kwamba kuanzishwa uhusiano na utawala wa Israel ndio 'msingi wa kupatikana amani halisi' katika Asia Magharibi. Kanali ya 13 ya televisheni ya utawala huo haramu pia ilitangaza mwezi Februari mwaka huu kwamba mfalme wa Bahrain ana hamu kubwa ya kuianzisha uhusiano wa wazi na rasmi na utawala huo.

Ama kuhusiana na hamu ya Bahrain ya kutaka kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel tunaweza kusema kuwa inatokana na:

Kwanza; Bahrain ndiyo nchi dhaifu zaidi kati ya nchi zote za Kiarabu kuhusiana na suala zima la usalama, ambapo si tu kwamba heshima na kujitawala hakuonekani sehemu yoyote katika siasa zake za nje, bali siasa hizo hubuniwa na kupangwa katika miji mikuu ya Washington na Riyadh. Kwa kweli hamu ya Bahrain kutaka kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel ni hamu ya Saudia kutaka kuwa na uhusiano rasmi na utawala huo, ila tu kwamba linaloiogopesha ni radiamali kali ya Waislamu na Waarabu dhidi yake kutokana na nafasi iliyonayo katika ulimwengu wa Kiislamu na wa Kiarabu, na ndio maana ikaamua kuisukuma mbele Bahrain katika uwanja huo. Katika kudumisha uhasama na uadui wake dhidi ya Iran, Washington pia inaona maslahi yake yakiwa katika kuzisukuma nchi za Kiarabu zianzishe uhusiano rasmi na utawala huo wa Kizayuni.

Pili; tokea Februari 2011 hadi sasa, utawala wa Aal Khalifa unakabiliwa na maandamano makubwa ya wananchi wa nchi hiyo kutokana na siasa zake za ukandamizaji na kuzitegemea nchi za nje katika kila jambo. Ili kupambana na maandamano hayo, utawala huo umeomba msaada wa nchi za Saudia, Marekani na utawala wa Kizayuni. Pande hizo zimekubali kuendelea kulinda usalama wa watawala wa Aal Khalifa dhidi ya wapinzani wa ndani kwa sharti kwamba waanzishe haraka uhusiano rasmi na wa wazi na utawala ghasibu wa Israel, na hivyo kuhafifishwa uovu wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo.

Ni zaidi ya miongo miwili sasa ambapo Bahrain imekuwa na uhusiano wa siri na utawala wa Tel Aviv, lakini sasa kuwekwa wazi na kutaka kuanzishwa uhusiano rasmi wa pande mbili ni jambo linalothibitisha wazi kuwa, watawala wa Manama wameamua kufuatilia kwa karibu hatua za kuanzisha haraka uhusiano huo ili wapate uungaji mkono wa Marekani na utawala katili wa Israel katika kukabiliana na wimbi la upinzani na maandamano ya Wabahrain ambao wanatilia shaka uhalali wa watawala hao.

Nukta ya mwisho ni kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahran anadai kwamba kuanzishwa uhusiano na Israel ndio msingi wa kupatikana utulivu na amani aya kudumu katika eneo katika hali ambayo ni wazi kuwa mslahi ya utawala huo ghasibu yanadhaminiwa kwa kuenezwa ghasia na machafuko katika Asia Magharibi na hasa ndani na baina ya nchi za Kiarabu.



/129